Jumatano , 25th Jan , 2023

Menejimenti ya Chuo cha Misitu Olmotonyi imetakiwa kubuni mikakati mipya ya kujiongezea mapato ili kuongeza udahili wa wanafunzi, motisha kwa wafanyakazi pamoja na kuzalisha mazao yatokanayo na misitu zikiwemo samani zenye ubora wa hali ya juu

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja ameyasema hayo leo katika kikao kilichofanyika kwenye ukumbi wa chuo hicho Jijini Arusha ambapo amesema kuna  haja ya kukiboresha chuo hicho ili kiweze kuleta tija kwa Taifa.

"Moja ya kazi ya kufanya ni kuendelea kubuni vyanzo vya mapato lakini pia ni lazima  muwe na maandiko mahususi yanayojenga hoja ili kuwafanya wanaotoa ukomo wa bajeti waweze kuliona kwa macho ya kipekee," amesema Naibu Waziri Masanja.

Amesema kuna haja ya kufanya mabadiliko hasa katika mfumo wa uendeshaji wa chuo hicho kwa kuwafundisha vijana vitendo zaidi kuliko nadharia ili kuwawezesha kuchakata mazao ya misitu yenye ubora wa hali ya  juu yatakayoweza kushindanishwa na bidhaa zinazotoka nje ya nchi.

Aidha, ameilekeza menejimenti hiyo kuzalisha vijana wakomavu na wenye taaluma ili wasaidie katika uhifadhi wa misitu kutokana na nchi kukumbwa na changamoto ya  uvamizi wa misitu na ukataji wa miti hovyo.

Katika hatua nyingine, Mhe. Masanja amesema Wizara  itaendelea kutatua changamoto zinazokikaboli chuo hicho ikiwa ni pamoja na kuongeza idadi ya watumishi na kuboresha muundo wa watumishi.

Awali, akiwasilisha taarifa ya utekelezaji Makamu Mkuu wa Chuo hicho , Stephen Kingwele amesema chuo kinakabiliwa na changamoto ya uhaba wa watumishi unaopelekea kuajiri watumishi wa mkataba ili kusaidia nguvukazi, pia ameishukuru Wizara ya Maliasili na Utalii ambayo imekuwa ikisaidia fedha za utekelezaji wa majukumu kupitia Mfuko wa Misitu.

Naye, Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Mhandisi Richard Ruyango amemshukuru Naibu Waziri kwa kufanya ziara katika chuo hicho kwa kuwa ndio mwanzo wa kutatuliwa kwa changamoto mbalimbali zinazokikabili.

Chuo cha Misitu Olmotonyi kilianzishwa mwaka 1937 kwa lengo la kuzalisha wafanyakazi katika sekta ya misitu ili kuwepo na uhifadhi endelevu.