Jumatano , 1st Jun , 2016

Rais wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amewahakikishia wafanyabiashara na wamiliki wa viwanda kuwa serikali yake itatoa ushirikiano wa kutosha kwa wenye viwanda na wenye nia ya kuanzisha viwanda vipya ili kufanikisha nia yake ya kuzalisha ajira .

Rais wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli

Rais Magufuli ametoa kauli hiyo jana katika hafla ya kutoa tuzo ya Rais kwa wazalishaji bora wa mwaka 2015, iliyofanyika Jijini Dar es salaam.

Dkt. Magufuli amesema serikali yake inatambua umuhimu wa viwanda katika uchumi na amewataka wenye viwanda na wenye nia ya kuanzisha viwanda kupuuza kauli zinazotolewa na baadhi ya watu wanaodai anawachukia wenye viwanda.

Amesema Rais Dkt. Magufuli huku akisisitiza kuwa serikali yake itafanyia kazi changamoto zilizotolewa na wenye viwanda zikiwemo miundombinu duni ya usafirishaji, nishati, mikopo na kodi pamoja na kuzuia uingizwaji holela wa bidhaa kutoka nje.

Rais Dkt. Magufuli pia ametoa wito kwa benki zinazoendesha shughuli zake hapa nchini kujenga mazingira bora kwa wanaohitaji mikopo kwa ajili ya kuanzisha viwanda ikiwemo kupunguza riba na amebainisha kuwa pamoja na kuimarisha Benki ya Uwekezaji (TIB), serikali yake pia inakusudia kuanzisha benki ya viwanda ili kuharakisha uanzishaji wa viwanda.

Amewahakikishia wenye viwanda kuwa serikali yake itavilinda viwanda vya ndani na kutaka wafanyabiashara wengi zaidi wajielekeza kuanzisha viwanda, badala ya kuendelea kuagiza bidhaa kutoka nje ya nchi licha ya malighafi nyingi kuwepo hapa hapa nchini.

Katika hafla hiyo, Rais Magufuli ametoa tuzo kwa washindi mbalimbali wa uzalishaji bora wa bidha za viwandani ambapo kampuni ya bia ya TBL imeibuka mshindi wa jumla.