Jumapili , 1st Oct , 2023

Wafanyabiashara wa soko la Karikaoo waliokuwa wakifanya biashara zao katika mitaa ya Big bon, Mafia na mtaa wa Mkunguni wamesema moto uliowaka maeneo hayo leo Oktoba Mosi, 2023, umewasababishia athari kubwa baada ya bidhaa zao zote kuteketea kwa moto.

Moja ya jengo likiwaka moto Kariakoo

Juhudi mbalimbali zimefanyikia na Jeshi la Zimamoto ili kudhibiti moto huo, ambapo hakuja ripotiwa athari zozote za kibinadamu kama vile majeruhi na vifo kutokana na moto huo 

"Tumeweza kudhibiti kusambaa kwa moto kwa haraka kwa sababu majengo mengi yameungana na hakuna nafasi ya kutosha baina ya jengo na jengo, Jeshi la Zimamoto limeweza kusaidia kupunguza athari za moto huu, niwasihi wafanyabiashara wa Kariakoo kuwa wastaarabu kwa sababu wapo wengine inapotokea shida kama hii wanadanganya kwamba maduka ni yao kumbe sio kweli," Edward Mpogolo, Mkuu wa wilaya ya Ilala

Kwa upande wake Kamanda wa Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji mkoa wa Ilala Elisa Mugisha, amesema kama kikosi cha zimamoto walipata taarifa mapema na walichukua tahadhari mapema za kudhibiti moto japo changamoto kubwa ni majengo mengi ya eneo hilo yameungana na sehemu zilizobaki za watu kupita pia zilikuwa na majengo hivyo imekuwa changamoto kwenye zoezi la uokoaji

Nao wafanyabiashara walioathirika na moto huo wameiomba serikali kuwasaidia kupambana na majanga hayo ya moto na athari walizozipata kwani wengi wao wana familia, mikopo na walikuwa wakitegemea biashara walizokuwa wakifanya maeneo hayo kuendesha maisha yao ya kila siku