Alhamisi , 11th Sep , 2025

Jeshi la Nepal litaendelea na mazungumzo na waandamanaji vijana nchini humo leo ya kumchagua kiongozi wa mpito wa taifa hilo.

Haya ni kwa mujibu wa msemaji wa jeshi, kufuatia maandamano yaliyosababisha vifo vya watu 30 na kusababisha waziri mkuu kuachia ngazi.

Jaji Mkuu wa zamani Sushila Karki ambaye ndiye aliyekuwa mwanamke wa kwanza wa Nepal kuteuliwa katika nafasi hiyo mwaka 2016, ndiye anayeongoza mbio za kuwa kiongozi wa mpito, kwa kuwa jina lake limependekezwa na idadi kubwa ya waliokuwa wakiongoza maandamano hayo.

Karki mwenye umri wa miaka 73 ameridhia ila vyanzo vilivyo karibu na mazungumzo hayo vinasema kwa sasa inatafutwa njia ya kikatiba ya kumteua.

Wanajeshi walikuwa wanapiga doria katika mitaa ya Kathmandu leo kufuatia maandamano mabaya zaidi kuwahi kutokea nchini humo kwa miongo kadhaa.

Maandamano hayo yalisababishwa na marufuku ya mitandao ya kijamii yaliyowekwa na serikali.