Jumatano , 24th Mei , 2023

Naomi Jeremiah (25), mkazi wa Kata ya Mabatini wilayani Nyamagana jijini Mwanza, amehukumiwa kifungo cha miezi minne gerezani au kulipa faini ya shilingi laki nne kwa kosa la kukutwa na lita 125 za pombe ya moshi maarufu kama gongo.

Naomi Jeremiah

Hukumu hiyo imetolewa katika Mahakama ya Mwanzo Nyamagana na Hakimu Mariam Omary baada ya kumtia hatiani mshtakiwa huyo kwa mujibu wa kifungu cha 32 cha kanuni ya mwenendo wa mashauri ya jinai ya mahakama za mwanzo jedwali la tatu, sheria ya mahakama na mahakimu sura ya 11 mapitio ya mwaka 2019.

Imeelezwa kuwa mnamo tarehe 11 ya mwezi huu Askari Polisi wakiwa kwenye doria eneo la mabatini walimkamata nyumbani kwake Naomi Jeremiah akiwa na pombe hiyo ya moshi lita 125 kisha kumpeleka kituo cha polisi na kumfungulia kesi namba 1239 ya kupatikana na pombe hiyo haramu.

Akitoa Ushahidi wake katika Mahakama ya Mwanzo Nyamagana Kaimu Mkuu wa Upelelezi wilaya ya Nyamagana aitwaye Makia Katani, aliyeongoza msako dhidi ya uhalifu na wahalifu ameiambia mahakama hiyo kuwa taarifa ya mshtakiwa kuhusika na biashara ya pombe hiyo haramu waliipata kutoka kwa wananchi ndipo wakaenda kukagua na kukamata lita 125 za pombe hiyo ya moshi.

Mara baada ya kufikishwa mahakamani mshtakiwa huyo alikiri kutenda kosa hilo ambapo mahakama ikamtia hatiani kwa mujibu wa kifungu cha 30 sheria namba 62 ya mwaka 1966, na kumfunga kifungo cha miezi minne gerezani au kulipa faini ya shilingi laki nne na kuamuru pombe hiyo kuharibiwa kwa kumwagwa.