Jumamosi , 16th Jun , 2018

Mbunge wa viti maalumu (CHADEMA), Upendo Peneza na Mbunge wa Temeke (CUF) Adallah Mtolea, wameisifu kampeni ya Namthamini ya East Africa Television na East Africa Radio kwa kusababisha kuondolewa kodi ya taulo za kike ili kurahisisha upatikanaji wake.

Akizungumza kwenye kipindi cha Weekend BreakFast kinachorushwa na East Africa Radio, Upendo Peneza amesema  mapendekezo yake yalipokelewa vizuri na serikali  na amefurahishwa na  hatua yakuondolewa kwa tozo hiyo  ambayo anaamini italeta unufaa wa kupatikana kwa taulo hizo.

''Wakati namuuliza Waziri Mkuu kuhusu mipango ya serikali yakurahisisha upatikanaji wa Taulo hizo, alinitaka nipeleke mapendekezo kwa Waziri wa Fedha , na pia nikashauriane naye kupata njia nzuri itakayosaidia upatikanaji wake, nilifanya hivyo na nashukuru wamefanyia kazi, lakini pia nawapongeza na nyinyi,  kwa juhudi mlizoonesha kuwasaidia watoto wasikose masomo yao", amesema Peneza.

Kwa upande wake Mbunge wa Temeke Abdallah Mtolea amekiri kufurahishwa na jambo hilo akiitaka serikali kuhakikisha wanasimamia utekelezaji wa kupunguza bei  kwa kuwa bado changamoto ya upatikanaji wa taulo hizo inaweza isiishe kwa kuondoa kodi pekee.

"Tunaona kama ni sehemu ya ushindi wa kampeni ya NAMTHAMINI, lakini hatuchukulii kama ni ushindi kabisa,  sababu bado tunahitaji kuwe na unafuu mkubwa wa upatikanaji wa hizo Pedi, tunahitaji serikali isimamie suala la kupunguzwa kwa bei ,  ili kuwabaini wafanyabiashara ambao watakuwa wakaidi", amesisitiza Mtolea.

Upendo Peneza mara kadhaa alishasimama Bungeni, akielekeza kilio chake kwa serikali kuhusu upatikanaji wa taulo za kike, wakati Abdallah Mtolea akiwa miongoni mwa wachangiaji wakubwa katika kampeni ya NAMTHAMINI,  iliyosimamiwa na EATV kwa kushirikiana na Msichana Intitiave ambapo asilimia kubwa ya fedha pamoja na taulo zilizokusanywa zimeshawafikia walengwa katika mikoa mbalimbali.