Jumatatu , 28th Sep , 2015

Makamu wa Rais wa Tanzania Dkt. Mohammed Gharib Bilal amewaongoza wakazi wa jiji la Dar es Salaam kuuaga mwili wa alieyekuwa Waziri wa nchi Ofisi ya Rais Menejiment ya Utumishi wa Umma Bi. Celina Kombani.

Makamu wa Rais wa Tanzania Dkt. Mohammed Gharib Bilal amewaongoza wakazi wa jiji la Dar es Salaam kuuaga mwili wa alieyekuwa Waziri wa nchi Ofisi ya Rais Menejiment ya Utumishi wa Umma Bi. Celina Kombani katika viwanja vya karimejee jijini Dar es Salaam, kabla ya kusafirishwa kwenda Morogoro kwa ajili ya maziko.

Akitoa salamu za rambirambi kwa niaba ya serikali waziri wa sera na uratibu wa Bunge Mh. Jenista Mhagama amesema familia ya Celina, wananchi wa Ulanga Mashariki, chama cha Mapinduzi na wananchi kwa ujumla ni wazi ameacha pengo kubwa kwa kuwa alikuwa ni muhimili muhimu katika maeneo yote hayo.

Aidha Mh. Mhagama amesema kuwa chama chake na serikali pia itamkumbuka Celina kutokana na utendaji wake kazi mahiri katika kuwatumikia wananchi wa jimbo lake na watanzania kwa ujumla katika kuwaletea maendeleo.

Aidha Mh. Mhagama ametoa taratibu za mazishi na kusema serikali pamoja na familia ya marehemu wamekubaliana kuwa mwili huo uzikwe nyumbani kwa marehemu mkoani Morogoro.

Kwa upande wake Spika anaemaliza muda wake Bi. Anna Makinda, akitoa Salamu za rambirambi kwa niaba ya bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amesema Mh. Celina wakati wa uhai wake na akiwa kama mbunge na akiwa kama Waziri alikuwa mchapakazi mahiri na pia msikivu ambae aliweza kutumia busara katika kutatua masuala muhimu ya kibunge na kiserikali.

Naye Makamu wa pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi visiwani Zanzibar Mh. Balozi Seif Idd amesema kuwa marehemu alikuwa ni mhimili na katika muungano wa Tanzania kwa kuwa waliweza kufanya naye kazi kwa ukaribu zaidi.

Kwa akitoa salamu za Rambirambi kwa niaba ya umoja wa wanawake wabunge nchini Bi. Angela Kairuki amesema kuwa umoja huo umepata pigo kubwa kwa kuwa alikuwa ni mmoja kati ya mihimili ya umoja huo ambapo wakati wa uongozi wake aliweza kuimarisha umoja huo.

Akisoma wasifu wa marehemu Naibu Katibu Mkuu wa Wizara aliyokuwa akiihudumia marehemu, Habib Mkwizu amesema Mh. Celina ametumika idara mbalimbali za serikali ambapo ameacha watoto watano wa kike wanne na mwanaume mmoja pamoja na wajukuu wanne.

Wakizungumza katika viwanja hivyo viongozi mbalimbali wa Kiserikali na kichama wametoa wasifu wa marehemu Kombani kwa kutanabiasha kuwa alikuwa mtu muhimu katika serikali na mtendaji kazi pamoja na ufuatiliaji wa masuala ya kiserikali na kwa wananchi kwa ukaribu zaidi.

Katibu wa NEC, Uchumi na Fedha Zakhia Meghji amesema serikali na Chama cha Mapinduzi kwa ujumla wamepata pigo kubwa kutokana na kuondoka kwa marehemu Celina kwa kuwa alikuwa kiungo muhimu kwa sehemu hizo mbili.

Celina Kombani alifariki dunia siku ya Alhamis Septemba 24 mwaka huu katika hospitali ya Apolo nchini India alikokuwa akipatiwa matibabu.