Wanakijiji wakiwa wamekusanyika nje ya nyumba kulimofanyika mauaji
Matukio ya mauaji ya kikatili dhidi ya wanawake katika wilaya ya Butiama yameanza kurejea upya baada ya mwanamke mmoja mkazi wa kijiji cha Maneke katika halmashauri ya Musoma mkoani Mara kuuawa kinyama kwa kukatwa mapanga tukio ambalo limehusishwa na imani za kishirikina.
Kamanda wa polisi mkoa wa Mara kamishna msaidizi wa jeshi la polisi ACP Philip Alex kalangi, amesema kuwa mwanamke huyo Mwadawa Elias mkazi wa kijiji hicho cha Maneke, ameuawa baada ya kuvamiwa akiwa amelala nyumbani kwake majira ya usiku na watu zaidi ya wanne kisha kuanza kumshambulia kwa kumkata kata kwa mapanga.
Mwanzoni mwa mwaka jana zaidi ya wanawake 40 katika tarafa ya Nyanja wilaya ya Butiama waliuawa kinyama kwa kuchinjwa na wengine kukatwa mapanga kisha wauaji kuchukua baadhi ya viungo vya miili ya marehemu kwa imani hizo za ushirikina na kusababisha hofu kubwa kwa jamii katika eneo hilo kabla ya hatua mbalimbali kuchukuliwa na serikali kupitia vyombo vyake vya dola katika kudhibiti ukatili huo.