Jumatano , 24th Nov , 2021

Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Tulia Ackson amesema serikali ipo kwenye utekelezaji wa mpango wa kutokomeza maambukizi ya Virusi vya UKIMWI nchini ifikapo mwaka 2030.

Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Tulia Ackson

Dk. Tulia ameyasema hayo leo Novemba 24, 2021 wakati akizindua wiki ya maadhamisho ya UKIMWI ambayo kitaifa inafanyika jijini Mbeya na kilele itakuwa ni Desemba 1, 2021 ambapo mgeni rasmi atakuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan.

''Tunaposema mwaka 2030 tunataka kutokomeza kabisa maambukizi ya UKIMWI ni mimi na wewe kujitokeza kupima ili kujua kama hauna maambukizi ujikinge lakini pia mwenye maambukizi naye apate zile dawa za kumpa afua,'' ameeleza Dk. Tulia Ackson.

Aidha, amewataka wananchi wa Mbeya kujitokeza kupima na kupata elimu kwa sababu mkoa huo una idadi kubwa ya maambukizi na unashika nafasi ya tatu kitaifa.

''Naomba sana wananchi wa Mbeya tujitokeze kushiriki kwenye kupima na kupata elimu kuhusu UKIMWI kama mnavyojua, takwimu zilizotajwa mkoa wa Mbeya ni wa tatu kitaifa kwa kuwa na idadi kubwa ya watu wanaoishi na maambukizi ya VVU,'' ameongeza Dk. Ackson.

Kituo cha Television cha East Africa kinarusha moja kwa moja matukio yote katika wiki hii hadi siku ya kilele cha maadhimisho hayo.