Watu watatu wamefariki dunia katika maeneo ya katika maeneo ya Mji Mpya, Mkundi na Mwembesongo katika manispaa na Mkoa wa Morogoro kutokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha mkoani humo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, SACP Alex Mkama katika taarifa aliyoitoa jana Desemba 30, 2025 amewataja waliofariki kuwa ni Lukman Chimbilo, aliyekuwa bodaboda, Onea Onesmo na Gervas Gerald, mwanafunzi aliyemaliza elimu ya darasa la saba mwaka 2025.
“Tukio la kwanza linahusiana na Lukman Chimbilo Ramadhan, mkazi wa Itigi kata ya Mwembesongo ambaye mnamo Disemba 19 majira ya jioni alifariki wakati akipatiwa matibabu baada ya kuangukiwa na waya unaodhaniwa kuwa ni umeme. Tukio hilo liliambatana na mvua kubwa ya upepo pamoja na radi. Uchunguzi bado unaendelea ili kubaini mazingira ya chanzo cha kifo chake, “amesema.
Kamanda Mkama amelitaja tukio la pili lililotokea mtaa wa Simu C kata ya Mji Mpya, Manispaa ya Morogoro ni lile la Disemba 20 majira ya usiku, ambapo Onea Onesmo mwenye umri wa miaka 50 alifariki wakati akipatiwa matibabu kutokana na kuangukiwa na ukuta wa nyumba aliyokuwa anaishi.
Katiaka tukio jingine, Gervas Gerald (13), mwanafunzi aliyemaliza elimu ya darasa la saba mwaka 2025 alifariki mnamo Disemba 29 katika bwawa la Sarawati kata ya Mkundi, Manispaa ya Morogoro ambaye licha ya mwili wake kuokolewa na kupelekwa hospitali alikumbwa na umauti.
Kufuatia matukio hayo, Kamanda Mkama amewahimiza wananchi kuchukua tahadhari zaidi na kuepuka maeneo hatarishi wakati wa kipindi hiki cha mvua zinazoendelea kunyesha katika sehemu mbalimbali za mkoa huo.

