Jumatano , 6th Apr , 2016

Wilaya ya Mtwara Mkoani Mtwara imeandaa mikakati ya kutokemeza suala la Uvuvi haramu tatizo ambalo limekithiri wilayani humo kwa kiasi kikubwa hali ambayo imechangia kupungua kwa upatikanaji wa Samaki.

Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Fatma Ally

Mikakati hiyo imetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Fatma Ally alipokua akizungumza na wavuvi wa wilaya hiyo ambapo amesema moja ya mikakati hiyo ni kuwataka wavuvi haramu kusalimisha zana zao kwa hiyari.

Aidha Mkuu huyo wa wilaya amesema kuwa wamepanga kuzunguka katika maeneo yote ya wilaya hiyo kwa wananchi wanaojihusisha na uvuvi ili kuwapa elimu ya madhara ya uvuvi haramu huku akisema kuwa wameanzisha msako maalumu kwa wavuvi watakaokiuka agizo lake.

Nao baadhi ya wavuvi walioshiriki katika Mkutano huo wameonyesha masikito yao kutokana na uvuvi huo haramu na kusema kuwa inafika wakati wanashinda baharini muda mrefu na kurejea nchi kavu na samaki kiduchu ambao hata mauzo yao hayatoshi kukidhi mahitaji yao.

Aidha wameongeza kuwa changamoto nyingine wanayokumbana na ni kukithiri kwa rushwa kwa baadhi ya watumishi wa serikali na matokeo yake kulifumbia macho suala hilo la uvuvi haramu na kuacha wavuvi hao kuendelea na uuzaji wa samaki ambao hawaruhisiwi kuvuliwa ikiwemo dagaa.

Sauti ya Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Fatma Ally akizungumzia mikakati ya kutokomeza uvuvi haramu Wilaya ya Mtwara.