
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi, na Mawasiliano, Injinia Isack Kamwelwe.
Waziri Kamwelwe ametoa kauli hiyo wakati akizungumza Jijini Dar es salaam ambapo alikiri kupungua kwa ajali za magari binafsi hususani kwenye kipindi cha mwisho wa mwaka lakini pia alibainisha kuwepo kwa ajali nyingi za magari ya serikali.
Waziri Kamwelwe amesema, "juzijuzi mliona ajali za magari ya serikali, tena ajali ambazo zilisababisha vifo vya wataalamu hasa wadogo, tena polisi wanatuheshimu sana magari ya serikali lakini mkituheshimu sana tutakufa. Kuna umuhimu wa magari ya serikali nayo yakafungwa kifaa maalum ili kudhibiti mwendokasi".
Aidha Waziri Kamwelwe amezitaka mamlaka zinazohusika na masuala ya usafiri nchini kuhakikisha kila mwananchi anakuwa na uhakika wa kutopata ajali itakayowapelekea ulemavu au vifo.
"Mimi huwa sipendi kusafiri mwezi wa wa 12 kwa sababu ajali zinakuwa ni nyingi sana, sasa kutakuwa na kidhibiti mwendo, ambacho kitatoa mipaka ya mwendokasi kwa madereva", ameongeza Waziri Kamwelwe.
Aidha Waziri Kamwelwe amesema msimamo wake ni kuwa atahakikisha hachukui likizo kwa kile alichokidai kuwa wapiga kura wake hawaendi likizo.