Ijumaa , 31st Mei , 2024

Mkakati mpya wa kuajiri walimu umetangazwa nchini Tanzania ambapo kwa sasa walimu ambao watakaopata ajira ni wale watakaofanya mitihani yao na kufaulu vizuri tofauti na ilivyokuwa awali ambapo wizara ya elimu ilikuwa ikijaza nafasi zilizokuwa zikihitajika bila kupitia mchakato huo.

Profesa Adolf Mkenda, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda amebainisha hayo Mei 30, 2024 Jijini Tanga wakati wa uwasilishaji wa taarifa ya hali ya ufaulu na ujifunzaji wa wanafunzi ulioshirikisha wadau mbalimbali wa elimu wakiwemo maafisa elimu mikoa, Halmashauri,Wakurugenzi na Taasisi

Alisema kwamba wanaoona jambo hilo sio jema kwao lakini wajiulize kwanini madaktari wanapomaliza Shahada ya kwanza wanalazimika kufanya mitihani ndio wanafanya kazi hivyo suala hilo linapelekwa kwa walimu ili kuweza kupata walimu bora.

Waziri  Profesa Mkenda alisema kwamba wanaamini kigezo hicho ndio ambacho kitalivusha Taifa na watahakikisha wanachukua walimu waliobora zaidi na watakaofanya mitihani na kufaulu vizuri.

 “Kama tunataka tuboresha elimu lazima twende kwa ujasiri tunapojaribu kuajiri walimu tujiulize tunapigania mwanao apata mwalimu bora sasa tutakapo ajiriw lazima wafanye mtihani na watakaofeli hawatapata nafasi”Alisema

Aidha alisema kwa sasa wapo kwenye mchakato wa Sheria mpya ambayo itawabana watu watakaobainika kuiba mitihani watakamatwa kushtakiwa kwa kesi za uhujumu uchumi na kwenye hilo niwashukuru Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA) kwa kufanya kazi nzuri wanayoifanya.

“Katika jambo hilo tuzidi kuwa makini tusijikuta tukazubaa tukaanguka Necta msilegeze kamba nendeni kuhakikisha mnalisimamia na  takwimu ni muhimu zitatueleza vizuri tunakwendaje na katika hilo tunataka kuimarisha takwimu za elimu Tanzania na kazi hii imeanza na timu ipo kazini”Alisema Waziri Profesa Mkenda

Awali akizungumza Katibu Mkuu Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia Prof Caroline Nombo alilipongeza Baraza la Taifa Mitihani (Necta) kwa taarifa yao ya uwasilishaji wa Taarifa ya Tathimini ya ujifunzaji kwa wanafunzi wa kidato cha pili.

Alisema kwamba taarifa iliyowasilishwa inatoa picha halisi kuhusu na ufundishaji na ujifunzaji  kwa shule za Sekondari na msingi nchini na mapendekezoo yaliyotolewa yanaonyesha dira ya nini cha kufanya  ili kuhakikisha ufundishaji na ujifunzaji na tathimini  katika ngazi ya shule unaimarika.

Naye kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani nchini (NECTA) Dkt Said Mohamed alisema suala la kufanya tathimini ni muhimu ili kuboresha kiwango cha elimu na wamekuwa wakifanya tathmini na mitihani na kueleza tahimini hiyo katika maeneo mbalimbali ni kutaka kujua maendeleo ya wanafunzi wamesoma na wanataka kufika wapi.

Alisema wamesema wameanza kufanya tathimini na masomo manne ambayo yameyafanya wakianzia na  somo la kwanza ni Hisabati,Sayansi huku akieleza kwamba katika somo hilo katika mtihani wa darasa la saba mwaka huu utakuwa hauna maswali ya kuchagua

Aidha alisema pia alisema hali ya ufauli nchini ukiangalia takwimu upimaji darasa la nne kwa miaka 10 uliopo ufaulu wa jumla umekuwa juu ya asilimia 80 itapanda kidogo na kushuka,miaka 10 hiyo utaona namna ya watahiniwa imekuwa ikiongezeka .

“Mfano mwaka 2015 darasa la nne laki tisa sasa kwenye usajili wanafikia mpaka 1,800,000 na ufaulu wameendelea kubakia 80 asilimia na namba ya watahiniwa imeongezeka mwaka hadi mwaka”Alisema

Katibu huyo alisema kwa upande wa Daraja la saba ulikuwa ni asilimia 67 mwaka 2015 na umeendelea kupanda na kufikia asilimia 80 mwaka 2023 kimahesabu huo ni ufaulu unaoafanana na bado wameendelea kufika asilimia 80 huku akieleza kwa upande wa Sekondari kidato cha pili ufaulu 2015 mpaka 2023 umekuwa ukiongezeka kutoka asilimia 67 2015 mpaka kufikia asilimia 89 mwaka jana.