Jumatano , 1st Apr , 2015

Mahakama ya Wilaya ya Dodoma jana ilimwachia mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara nchini, Johnson Minja kuendelea na dhamana yake baada ya kujiridhisha kuwa hakuvunja masharti ya dhamana yake tangu aliapoachiwa kwa dhamana Januari 28 mwaka huu.

Minja, (Kulia), akiongozana na wakili wake, Godfrey Waonga wakati akiwasili mahakamani mjini Dodoma.

Hakimu mfawidhi wa mahakama ya Wilaya ya Dodoma, Rhoda Ngimilanga amesema kuwa ameridhishwa na upande wa utetezi kuwa mshitakiwa hajawahi kuvunja masharti ya dhamana yake tangu alipoachiwa kwa dhamana Januari 28 mwaka huu.

Awali mwendesha mashtaka mwandamizi wa serikali, Rose Shio aliiambia mahakama kuwa upelelezi wa kesi hiyo umeshakamilika ambapo April 9 itaanza kusikilizwa kwa usikilizwaji wa awali.

Hata hivyo aliiomba mahakama hiyo kuendelea kuzuia dhamana ya Mshtakiwa kwa kuwa bado hapakuwa na utulivu wa amani nje kutokana na wafanyabiashara kuendeleza migomo ya kufungua maduka yao pamoja na kugoma kuendelea kutumia mashine za kieletroniki za Efds.

“Pamoja na kukamilika kwa upelelezi wa kesi hiyo lakini mshtakiwa ameendelea kukiuka masharti ya dhamana aliyopewa Januari 28 mwaka huu kwa hiyo tunashauri mahakama iendelee kuzuia dhamana ya mshtakiwa hadi pale hali ya amani itakapotengemaa katika mji wa Dodoma,” alisema Shio na kuongeza kuwa,

“Bado kuna hali ya tahadhari katika mji wa Dodoma, biashara bado haziendelei na pia bado kuna mgomo wa kufungua maduka, na utumiaji wa mashine za kukusanya kodi za efds ambapo kwa sasa hali imekuwa ni mbaya zaidi kwa hiyo tulikuwa tunashauri kuwa mshtakiwa arudi ndani hadi hali ya usalama itakapotengemaa.”

Kwa upande wake wakili wa mshtakiwa, Godfrey Wasonga aliipinga hoja ya wakili wa serikali kwa kusema kuwa mshtakiwa huyo ana haki ya kupata dhamana kama ilivyo kwa makosa mengine ya jinai na kwamba kuendelea kumshikilia ni kuvunja katiba ya nchi.

“Napenda kuiambia mahakama yako tukufu kuwa tangu mshtakiwa aachiwe kwa dhamana hajawahi kuvunja sharti hata moja la dhamana yake,” alisema Wasonga

Alisema na hoja ya serikali kuwa anaitisha mikutano ya kuwazuia wafanya biashara kugoma kutumia mashine za kieletroniki za efds alisema kuwa katika masharti ya dhamana yake hakukatazwa kuitisha mikutano na wala hajawahi kuwazuia wafanyabishara nchini kutumia mashine za kukusanya kodi za EFDs.

Pia alisema kuwa hoja ya kwamba mshtakiwa aendelee kukaa gerezani mpaka amani itakaporejea alisema kuwa jukumu la kulinda amani ya mahali husika ni la serikali na siyo jukumu la Minja.

“Sasa kama Minja ataendelea kukaa ndani atajuaje kama Tabora, Tanga, Arusha na Mbeya maduka yamefunguliwa?” alihoji Wasonga na kuongeza kuwa,

“Mheshimiwa hakimu najua kuwa mahakama ndiyo chombo pekee cha kutoa haki na usiendelee kusikiliza taarifa za umbea umbea kutoka kwa wakili wa serikali.”

Aliishauri mahakama kumwachia huru mshtakiwa kwa masharti ya mwanzo ili aendelee kufanya shughuli zake.

Masharti ya mwanzo ya dhamana aliyopewa Minja ni kuwa na wadhamini watatu ambapo mmoja kati ya hao ni lazima awe ni mfanyakazi wa serikali ambaye anaishi mkoani Dodoma.

Akijibu hoja hizo Hakimu Ngimilanga alisema kuwa hoja ya wakili wa serikali kuwa Minja alikuwa anaitisha mkutano ya kuwazuia wafanyabishara haina mashiko kwa kuwa kama alifanya hivyo sheria inasema kuwa angekamatwa muda huo huo na kwamba hilo halikuwa miongoni mwa masharti ya dhamana yake.

Alisema kuwa mshtakiwa ataendelea kuwa nje kwa dhmana hadi April 9 mwaka huu ambapo kesi hiyo itatatjwa tena kwa usikilizwaji wa awali.