Ijumaa , 24th Mei , 2024

Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Mohamed Salim Ratco ametilia mashaka mradi wa ujenzi wa stendi ya mabasi Mombo kutokana na fedha kiasi cha shilingi milioni 30 zilizotolewa kutumika bila matumizi yaliyokusudiwa ikiwa ni pamoja na makisio ya mradi huo kutoonyesha uhalisia sahihi.

Kufuatia hatua hiyo MNEC Ratco amemuagiza Mkurugenzi wa Halmshauri ya Korogwe Vijijini kuhakikisha ujenzi wa kituo cha mabasi Mombo unakamilika na kuanza kutumika ifikapo tarehe 1 mwezi julai mwaka huu. 

Ujenzi wa kituo hiko cha mabasi ambao serikali imetoa kiasi cha shilingi Millioni 38 ulipaswa ukamilike tarehe 6 mei mwaka 2024 lakini mpaka sasa ujenzi huo bado haujakamilika.

Akizungumza mara baada ya kutembelea eneo mradi unapotekelezwa MNEC Ratco amesisitiza hadi kufikia tarehe 1 julai ujenzi uwe umekamilika kwa viwango na ubora unaotakiwa bila kuweka visingizio vyovyote. 

"Natoa masikitiko yangu kuhusu hali ya stendi hii hapa inaonekana kuna tatizo na ndio maana Mwenyekiti wa Halmashauri pamoja na mheshimiwa DC mmeongea hapa lakini inaonekana stendi hii ni tatizo kweli kweli tulishapoteza nyuma milioni 30 za makinikia je mlichukua hatua gani nikiuliza kwa wale ambao walitengeneza lakini pamoja na hayo kuna milioni 38 zilizotengwa kwajili ya ujenzi wa kifusi kitu ambacho mimi kinanitia mashaka je na zenyewe zikipotea tunafanyaje sasa tuangalie suala hili lisije kuondoka na mtu, "alisema MNEC. 

"Hawa wakandarasi kama hawatokuwa na ujenzi wenye ubora chini ya mwaka mmoja hatua gani zinachukuliwa maana zisichukuliwe tu hatua kwenye makaratasi wanawajibika kwa njia gani wito wangu stendi hii ikamilike tarehe moja mwezi wa saba lakini iwe na ubora usiopungua mwaka mmoja kama ulivyoahidi Mwenyekiti wa Halmashauri, "alisema MNEC Ratco. 

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Korogwe Simon Mwakilema ameahidi kusimamia ujenzi wa mradi huo ipasavyo na kuhakikisha unakamilika kwa wakati uliopangwa huku wananchi wakiiomba serikali kujenga kituo kitakachokidhi mahitaji ya wananchi ikiwemo uwepo wa vizimba vya biashara.

Katika ziara yake wilayani Korogwe Mjumbe wa Halmashauri Kuu CCM Taifa ametembelea na kukagua ujenzi wa zahanati pamoja ujenzi wa vyumba vya madarasa na vyoo katika shule za sekondari Mnyuzi na Mwisho wa Shamba.