Mkuu wa wilaya ya Bukombe Paskasi Muragili
Katika Halmashauri ya wilaya ya Bukombe mkoani Geita hatimiliki zisizopungua 30,827 zitatolewa kwa lengo la kuboresha miliki za ardhi za wananchi ili kuchochea maendeleo ya wilaya, kuleta usalama wa miliki za ardhi, kukukuza uchumi na kupunguza au kumaliza migogoro itokanayo na ardhi.
Hayo yamebainishwa na Mkuu wa wilaya ya Bukombe Paskasi Muragili wakati wa ufunguzi wa kikao cha kujadili utekelezaji wa mradi wa LTIP katika Halmashauri ya wilaya ya Bukombe.
Aidha Mkuu wa wilaya huyo amewaagiza viongozi wote katika wilaya hiyo kutoa ushirikiano kwa wataalam pindi zoezi hilo litakapoanza pamoja na kutoa elimu kwa wananchi wanaowasimamia juu ya uwepo wa mradi huo na manufaa yake.
Mtendaji Kata wa Lyambambongo Jacob Raphael amesema kuwa uwepo wa mradi huo utasaidia kupunguza au kumaliza kabisa migogoro ya ardhi na kupelekea wananchi kupata hatimiliki za maeneo yao itakayowasaidia kupata mikopo kwenye taasisi za kifedha.
Utekelezaji wa mradi huo unahusisha utambuzi wa kila kipande cha ardhi, upangaji wa maeneo yote yaliyotambuliwa kwa kuandaa michoro ya mipangomiji, upimaji wa viwanja vilivyopangwa kwa kuweka alama za upimaji na kuandaa ramani za upimaji na wananchi kumilikishwa maeneo yao kwa kupewa hatimiliki.