Alhamisi , 22nd Mei , 2014

Wafanyakazi wa Mamlaka ya Reli Tanzania na Zambia (TAZARA) wameendelea na mgomo licha ya serikali kutangaza kuwalipa mishahara ya mwezi Februari na Aprili, ambapo wamesisitiza ni lazima walipwe mishahara yao yote kwanza.

Moja ya treni inayomilikiwa na Shirika la Reli kati ya Tanzania na Zambia (TAZARA). Kwa muda sasa usafiri wa mizigo na abiria kati ya Dar es Salaam na Lusaka umekwama kutokana na mgomo wa wafanyakazi wa shirika hilo.

Msimamo wao huo umetolewa baada ya Meneja wa TAZARA upande wa Tanzania Mhandisi Abdalah Sekimwezi kuwasilisha taarifa kutoka kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, na kueleza kuwa wametoa mishahara waliyokuwa wanadai ya mwezi Februari na Aprili, ambapo upande wa Zambia nao utalipa Mwezi Machi na Mei.

Hata hivyo wafanyakazi hao kupitia Katibu wa Chama cha Wafanyakazi wa Reli (TRAWU), Erasto Kihwele wamesema kuwa hawapo tayari kurejea na kazi hadi hapo watakapolipwa mishahara yao yote huku wakitaka TAZARA upande wa Tanzania kupewa madaraka kamili ili ijiendeshe kwa kujitegemea bila ya Zambia.