Rais wa Marekani Donald Trump, pamoja na marais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Rwanda, Félix Tshisekedi na Paul Kagame, wamesaini makubaliano ya amani huko Washington siku ya jana Alhamisi, Desemba 4, 2025, huku mapigano makali yakiendelea kurindima katika maeneo mbalimbali mashariki mwa DRC.
Rais wa Marekani ameuita mkataba huo maarufu kama maarufu kama ‘The Washington Accord’ kuwa ni muujiza mkubwa huku Rais wa Rwanda, Paul Kagame, akionya kwamba kutakuwa na heri na hasara katika utekelezaji wa mikataba ya Washington.
"Ni jukumu letu barani Afrika kufanya kazi na washirika wetu ili kuimarisha na kupanua amani hii", alisema Kagame.
Kwa upande wake Félix Tshisekedi kutoka DRC, ameusifu mwanzo wa njia mpya.
Akiwazungumzia viongozi hao wawili kutoka Afrika Mashariki, Trump amesema walitumia muda mrefu kuuana, ila kwa sasa watatumia muda wao kufurahi pamoja, hususani wakifaidi matunda ya kiuchumi ya Marekani.
Kulingana na Trump, mkataba huo utatoa fursa kwa Marekani kuanza kuchimba madini adimu yanayopatikana DRC na Rwanda.
Utiaji saini wa mkataba huo wa amani unakuja miezi mitano, baada ya mawaziri wa mambo ya nje wa Rwanda na DRC kukutana na Rais Trump, na kuonesha nia yao ya kumaliza mapigano.

