Alhamisi , 8th Dec , 2016

Mfumuko wa Bei wa Taifa kwa mwezi Novemba 2016 umeongezeka hadi kufikia asilimia 4.8 kutoka asilimia 4.5 iliyokuwapo  mwezi Oktoba, 2016 kutokana na kuongezeka  kwa bei ya bidhaa na huduma katika maeneo mbalimbali nchini.

Mkurugenzi wa Sensa na Takwimu za Jamii wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Bw. Ephraim Kwesigabo

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam, Mkurugenzi wa Sensa na Takwimu za Jamii wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Bw. Ephraim Kwesigabo amesema kuwa bidhaa za vyakula zikiwemo ngano,mbogamboga, mtama,  na vinywaji baridi zimechangia kuongezeka  kwa mfumuko wa bei nchini.

“Bidhaa nyingine zilizochangia kuongezeka kwa mfumuko wa bei nchini ni Nishati , mafuta  na viatu huku akibainisha kuwa kipimo kinachotumika kupima mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma zinazotumiwa na kaya nchini zimeongeka na kufikia 104.32 kwa mwezi Novemba 2016 ikilinganishwa na 99.54 za mwezi Novemba  mwaka jana” Alisema Kwesigabo.

Aidha, amesema kuwa thamani ya shilingi ya Tanzania hupima badiliko katika kununua bidhaa na huduma zilezile za mlaji ambazo shilingi ya Tanzania ingeweza kununua katika kipindi tofauti, ikiwa fahirisi za bei za taifa zinaongezeka uwezo wa shilingi ya Tanzania katika kununua bidhaa na huduma hupungua.

Kwa upande wa mfumuko wa bei wa Tanzania na baadhi ya nchi za Afrika Mashariki Kwesigabo amesema  kuwa una mwelekeo unaofanana ambapo Kenya umeongezeka  na kufikia asilimia 6.68 mwezi Novemba kutoka 6.42 za mwezi Oktoba huku Uganda ikiwa na mfumuko wa bei wa asilimia 4.6 mwezi Novemba kutoka asilimia 4.5 za mwezi Oktoba.