Jumatatu , 11th Dec , 2017

Mstahiki Meya wa Jiji la Dar es salaam Isaya Mwita, anatarajia kuzungumza katika mkutano wa kujadili changamoto zinazo wakabili viongozi wa serikali za mitaa, ulioandaliwa na Umoja wa Mataifa jijini Addis Ababa nchini Ethiopia.

Mkutano huo wa siku tatu unaanza leo na unatarajiwa kujadili na kutoa majibu ya changamoto mbalimbali ambazo wanakutana nazo viongozi wa serikali za mitaa wakiwemo Mameya.

Meya Mwita ameondoka nchini jana jioni kuelekea  Addis Ababa, ambapo katika mkutano huo atazungumza kuelezea changamoto zilizopo katika jiji la Dar es Salaam na namna ambavyo  kwa asilimia kadhaa wameweza kuzitatua.

Mbali na Mameya, mkutano huo pia utahudhuriwa na viongozi wengine wa serikali za mitaa kutoka Nchi mbalimbali duniani. Lengo kuu ni viongozi hao kujadili changamoto zinazozikabili halmshauri zao, mafanikio, lakini pia kujengeana uwezo kwenye utendaji kazi.

Miongoni mwa changamoto ambazo mkutano huo utajikita katika kuzijadili ni suala la bajeti katika halmashauri na ukusaji wa mapato ambavyo ndio msingi wa maendeleo.