Jumatatu , 19th Feb , 2018

Mbunge wa Australia George Robert Christensen amejikuta akikabiliwa na wakati mgumu pamoja na shutuma baada ya kutuma picha kwenye ukurasa wake wa Facebook akiwa na bastola huku akidaiwa kutoa maneno ya kejeli kwa wafuasi wa Chama cha Green.

Maneno yanayodaiwa kuambatanishwa na picha hiyo yamesomeka "mnahisi mna bahati,ninyi watu msio na thamani" (“Do you feel lucky, greenie punks?”)

Chama cha Green kimesema kwamba kauli iliyotolewa na mbunge huyo wa Chama cha Conservative ni ya kusikitisha sana na kuainisha kwamba ameitoa kipindi ambacho watu 17 wameuwawa nchini Marekani katika shambulio la bunduki katika shule moja jimboni Florida..

Polisi katika mji huo imesema kwamba inaangalia uwezekano wa ikiwa uchunguzi unaweza kufanyika au la ingawa mbunge huyo amekaririwa akisema kwamba kauli hiyo aliyoituma ilikuwa utani.

Waziri Mkuu wa nchi hiyo  Malcolm Turnbull amesema kauli hiyo iliyotumwa katika ukurasa wa facebook wa mbunge huyo haikuwa sahihi.

Taarifa nyingine kutoka makao makuu ya jeshi la polisi nchini humo imesema inapima kauli hiyo kabla ya kuchukua hatuahuku Wapinzani wa kisiasa wakimshutumu  Christensen kwa kuchochea vurugu.