Alhamisi , 2nd Mar , 2017

Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imetupilia mbali maombi yaliyowasilishwa na Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe ya kutaka asikamatwe na polisi mpaka pale kesi yake ya kikatiba dhidi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda itakapomalizika

Freeman Mbowe

 

Sababu ya maombi hayo kutupwa imeelezwa kuwa ni kutokana na kukosewa kwa kifungu cha sheria kilichotumika ambapo mahakama imemtaka mleta maombi kufanya marekebisho katika maombi yake.

Akizungumza na wanahabari, Mbowe amesema wanakwenda kurekebisha yale waliyoambiwa ili waweze kuendelea mbele.

"Tunakwenda kufanya marekebisho kwa yale tuliyoambiwa na mahakama turekebishe, baada ya kumaliza hapa tunaelekea Arusha kusikiliza kesi ya Godbless Lema ya kupata dhamana". Alisema Mbowe

Katika hatua nyingine, mwanahabari nguli nchini Jenerali Ulimwengu, ameungana na jopo la mawakili Tundu Lissu, Peter Kibatala na John Mallya katika kumtetea Mbowe ambaye amesema kuwa marekebisho yao yatawasilishwa siku ya Ijumaa Machi 3.

Kutoka kushoto, Freema Mbowe, Jenerali Ulimwengu na Meya wa Ubungo, Boniface Jacob

"Kesi kimsingi bado ipo palepale itasikilizwa tarehe 8 Machi mwaka huu, tutaleta marekibisho yetu yakichelewa sana itakuwa kesho Ijumaa na hatuwezi kuleta marekebisho yetu mpaka kwanza tuone maamuzi yenyewe ya majaji ili tusome vizuri tuelewe vizuri ili tuweze kujua marekebisho yenyewe yapo wapi". Amesema Jenerali Ulimwengu

Mbowe amefungua kesi hiyo ya kikatiba namba 1, ya mwaka 2017 dhidi ya wadaiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam na Ofisa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Kanda Maalumu ya Dar es Salaam.