
Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limewatoa hofu wananchi kuhusu taarifa iliyozua taharuki kwenye mitandao ya kijamii ikidai kuwa mabaki ya viungo vya binadamu yamekutwa eneo la Magole Mpiji, Kwenye taarifa yake jeshi la polisi limesema kuwa taarifa hiyo ni ya zamani takribani miaka 11 na si tukio jipya.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Julai 24, 2025 na Kamanda wa Polisi wa Kanda hiyo SACP Jumanne Muliro imesema “Taarifa ya tukio hilo ni ya zamani miaka 11 iliyopita na ilitolewa ufafanuzi wake tarehe 22.7.2014 na aliyekuwa Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es salaam wakati huo”, imesema sehemu ya taarifa hiyo.
Polisi wamesema kuwa katika tukio hilo, watu wanne wakiwemo madaktari na wataalamu kutoka Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Tiba na Teknolojia (IMTU) walikamatwa kufuatia taarifa kutoka kwa wananchi kuhusu kuwepo kwa viungo vya miili ya binadamu vilivyotupwa katika bonde la Mto Mbezi eneo la Magole Mpiji, Kinondoni.
Uchunguzi uliohusisha Jeshi la Polisi, Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Wizara ya Afya na taasisi nyingine za uchunguzi ulibaini kuwa viungo hivyo vilitolewa kwenye maabara ya mafunzo ya IMTU na kutupwa kinyume cha taratibu.
Waliokamatwa walifikishwa mahakamani mbele ya Hakimu Mfawidhi wa wakati huo, Kwey Rusema, ambapo Wakili wa Serikali Magoma Mtani aliwasomea mashtaka yanayohusiana na utupaji huo haramu wa mabaki ya miili ya binadamu.
Aidha Jeshi la Polisi limeonya kuwa halitasita kuchukua hatua za kisheria dhidi ya watu wanaosambaza taarifa za uongo au zenye lengo la kuzusha taharuki miongoni mwa wananchi.