Jumanne , 18th Feb , 2025

Mazungumzo kati ya ujumbe wa Urusi na Marekani yameanza huko Saudi Arabia, kwa ajili ya kutafuta suluhu na kumaliza vita vya Ukraine.

Kwa upande wa Marekani unasisitiza kwamba mazungumzo hayo sio kuanza makubaliano, lakini ni kufanyia kazi iwapo Urusi ina dhamira ya dhati ya kumaliza vita vya Ukraine.

Urusi inasema kipaumbele chake ni kuboresha mahusiano yake na Marekani.
Mkutano huu ni wa ndani na haifahamiki utachukua muda gani.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, Balozi wa Marekani katika Mashariki ya Kati, Steve Witkoff, na Mshauri wa Usalama wa Taifa, Mike Waltz, wote wamewasili katika nchi hiyo ya Ghuba kwa ajili ya mazungumzo ya awali.

Kwa upande wa Urusi, Waziri wa mambo ya nje, Sergei Lavrov, pamoja na mshauri wa Rais Vladimir Putin, Yuriy Ushakov, wanashiriki katika mazungumzo hayo, kwa mujibu wa vyombo vya habari vya serikali ya Urusi.

Watendaji hao wanawawakilisha Trump na Putin, kufuatia mazungumzo ya awali kwa njia ya simu kati ya viongozi hao yaliyofanyika wiki iliyopita. Baada ya mazungumzo hayo Trump alisema anatarajia kukutana na Vladimir Putin "hivi karibuni."

Hata hivyo Ukraine haijaalikwa kushiriki katika mazungumzo haya yanayofanyika Riyadh, jambo ambalo limezua wasiwasi miongoni mwa viongozi wa Ulaya. 

Katika hatua nyingine Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, amesema kuwa amezungumza na Rais wa Marekani Donald Trump na na mwenzake wa Ukraine, Volodymyr Zelensky ili kuwafahamisha kuhusu yaliyojiri kwenye mkutano wa viongozi wa Ulaya uliofanyika jana huko Paris.

Viongozi wa Uingereza na wa EU walikutana kwenye mkutano wa dharura kuhusu Ukraine hapo jana. 
Bado haijulikani nini kilijadiliwa, lakini ripoti zinaonyesha kwamba nchi zilizoshiriki zilikuwa zimegawanyika kuhusu kama Ulaya itawapeleka wanajeshi wa amani huko Ukraine iwapo kutakuwa na makubaliano ya kusitisha mapigano.