Mawaziri mbalimbali waliojitokeza hii leo kuchukua fomu katika maeneo yao, akiwemo Profesa Kabudi, Profesa Ndalichako, Angellah Kairuki na Dkt Philip Mpango.
Katika baadhi ya Mikoa wameshuhudiwa baadhi ya Mawaziri wa Serikali ya awamu ya tano wakijitokeza kuomba ridhaa ya kutetea majimbo yao, huku wengine ikiwa ndiyo mara yao ya kwanza.
Mkoani Kagera, Waziri wa Viwanda na Biashara Innocent Bashungwa, amefika kwenye Ofisi za Chama cha Mapinduzi wilaya ya Karagwe kuchukua fomu ya maombi ya kugombea nafasi ya Ubunge wa jimbo la Karagwe.
Naye Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga, amechukua fomu ya kugombea Ubunge wa Jimbo la Vwawa Mkoani Songwe, kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi akitetea kiti chake kwa awamu ijayo ya miaka mitano.
Kwa upande wa Mkoa wa Pwani Waziri wa TAMISEMI Selemani Jafo, leo Julai 14, 2020, amechukua fomu ya kuomba ridhaa chama chake ili kimteue kwa ajili ya kugombea Ubunge wa Jimbo la Kisarawe. Jafo ameijaza fomu palepale na kisha kuirejesha.
Huku na kule Kigoma ameshuhudiwa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof Joyce Ndalichako, akichukua fomu ya kuomba ridhaa chama chake ili kiweze kumteua, aweze kugombea Ubunge katika jimbo la Kasulu Mjini kupitia CCM.
Kwa upande wake, Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango, amechukua fomu ya kuomba kuteuliwa na Chama cha Mapinduzi kuwania Ubunge jimbo la Buhigwe mkoani Kigoma.
Aidha kwa upande wa Kilimanjaro, Waziri wa Nchi ofisi ya Waziri Mkuu-Uwekezaji Angellah Kairuki, amechukua fomu ya kuomba kuteuliwa na CCM kuwania ubunge Jimbo la Same Magharibi katika uchaguzi Mkuu mwezi Oktoba.
Waziri Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Profesa Palamagamba Kabudi, naye hakuwa nyuma, ambapo amechukua fomu ya kuomba ridhaa chama chake ili kiweze kumteua, aweze kugombea Ubunge katika jimbo la Kilosa mkoani Morogoro





