Jumatano , 23rd Nov , 2016

Mawakili wa Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema wamesajili maombi ya rufaa namba 112/113 ya mwaka 2016 Katika Mahakama kuu Kanda ya Arusha, ili kudai haki ya dhamana ya Mbunge huyo.

Godbless Lema - Mbunge wa Arusha Mjini

 

Akizungumza leo Jijini Arusha Mawakili hao ambao ni Sheck Mfinanga na Peter Kibatala wamesema tayari wamesajilia Mahakama kuu rufaa yao na wanasubiri kupangiwa Jaji wa kusikiliza rufaa yao.

Wamesema wameamua kufungua maombi ya rufaa kwaajili ya kujua ni kwanini Lema amekosa dhamana ambayo awali Hakimu Desdery Kamugisha alisema ipo wazi.

Aidha wamesema sababu ya kufungua rufaa hiyo ni kwamba hawakuridhishwa na hatua ya Hakimu Kamugisha kumnyima dhamana Lema, huku akijua kuwa alifanya kosa kwa sababu mawakili wa serikali akiwemo Paul Kadushi walisema wameonyesha nia ya kukata rufaa.

Wakili Peter Kibatala

Wamesema wanapinga Lema kunyimwa dhamana iliyo wazi na ndio maana wameamua sasa kukata rufaa na wanasubiri Mahakama Kuu kuwapangia Jaji wa kusikiliza maombi ya rufaa yao.