Jumatatu , 4th Sep , 2023

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt. Doto Biteko ameikabidhi Ofisi ya Wizara ya Madini kwa Anthony Mavunde ili aanze rasmi kazi ya kuiongoza Wizara hiyo.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt. Doto Biteko akimkabidhi nyaraka Waziri mpya wa Wizara ya Madini Anthony Mavunde

Makabidhiano hayo yamefanyika leo Septemba 4, 2023 katika Ofisi za Wizara ya Madini jijini Dodoma ambapo Dkt. Biteko ametumia fursa hiyo kumkabidhi Waziri Mavunde  vipaumbele vya Wizara ya Madini kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024.

Vipaumbele alivywasilisha Dkt.Biteko ni pamoja na kuimarisha ukusanyaji wa maduhuli na kuongeza mchango wa sekta ya madini kwenye Pato la Taifa, kuendeleza madini muhimu na madini mkakati, kuhamasisha shughuli za uongezaji thamani madini na kuhamasisha uwekezaji na biashara katika sekta ya madini.

Vipaumbele vingine ni uanzishwaji wa minada na maonesho ya madini ya vito, kuwaendeleza na kusogeza huduma za ugani kwa wachimbaji wadogo na kuzijengea  uwezo taasisi zilizo chini ya Wizara ya Madini ili ziweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

Dkt. Biteko ametumia fursa hiyo kuwashukuru viongozi na Watumishi wa Wizara ya Madini na Taasisi zake kwa ushirikiano mkubwa waliomuonesha katika kipindi chake cha utekelezaji wa majukumu mbalimbali.

Kwa upande wake, Waziri wa Madini Anthony Mavunde amesisitiza kuwa ataonesha ushirikiano kwa watumishi wa Wizara ili kufikia malengo yaliyowekwa kwa Mwaka wa Fedha 2023/24.

Naye, Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa amemshukuru Dkt. Biteko kwa ushirikiano aliompatia katika kipindi walichofanya kazi pamoja na kumtakia Kheri katika majukumu yake mapya.