Alhamisi , 21st Jan , 2016

Aliyekuwa mbunge wa bunge la 10 la Jamhuri ya muungano wa Tanzania, marehemu Lecia Nyerere amezika leo, wilayani Butiama mkoani Mara.

Maelfu ya wananchi wa mkoa wa Mara na mikoa jirani ya kanda ya ziwa wakiwemo viongozi mbalimbali na vyama vya siasa wameshiriki katika mazishi ya aliyewahi kuwa mbunge wa bunge la jamhuri wa muungano wa Tanzania marehemu Leticia Nyerere katika kijiji cha Butiama mkoani Mara.

Katika mazishi hayo ambayo yamefanyika eneo la Mwitongo kijijini Butiama , serikali imewakilishwa na mkurugenzi wa utawala na utumishi kwa niaba ya katibu mkuu ofisi ya Rais, menejimenti ya utumishi wa umma bwana Aloyce Msigwa huku ofisi ya bunge ikiwakilishwa na mkurugenzi msaidizi wa huduma kwa wabunge Bw Seleman Mvunye kwa pomoja wametoa pole kwa familia ya baba wa taifa mwalimu Julius Kambarage Nyerere kufuatia msiba huo.

Kwa upande wao baadhi ya wanasiasa na wabunge wa bunge la Jamhuri ya Janzania na wale kutoka bunge la Afrika Mashariki, wakitoa salamu zao katika mazishi hayo wakimwelezea marehemu Leticia Nyerere kuwa ni moja ya wanasiasa waliopenda ushirikiano hasa kwa kujenga hoja zenye maslahi kwa taifa.

Naye jaji Aisha Makongoro Nyerere, akisoma wasifu wa marehemu, amesema Leticia Mageni Nyerere alizaliwa tarehe moja mwezi Machi mwaka 1959 katika kijiji cha Kitunga wilayani Kwimba mkoani Mwanza.

Katika mazishi hayo ambayo yalitanguliwa na ibada ya mazishi iliyofanyika katika Parokia ya Butiama, viongozi mbalimbali akiwemo mama Maria Nyerere na mkuu wa majeshi mstaafu David Msuguri wamepata fursa ya kuweka mashada ya maua katika kaburi la marehemu Leticia Mageni Nyerere.