Ijumaa , 2nd Oct , 2020

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, limesitisha wito wake kwa mgombea urais kupitia CHADEMA Tundu Lissu na kumtaka aendelee na kampeni zake kama kawaida lakini maagizo na wito wa IGP Simmon Sirro, wa kumtaka aripoti polisi mkoani Kilimanjaro uko palepale.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, SACP Lazaro Mambosasa.

Kauli hiyo imetolewa na Kamanda wa Polisi wa kanda hiyo Lazaro Mambosasa, wakati akizungumza na EATV&EA Radio Digital, na kusema kuwa waliamua kumuandikia barua ya wito Tundu Lissu, kufika Dar es Salaam kwa lengo la kumhoji.

"Tumesitisha kwa sababu kile alichokuwa anaitiwa tayari IGP alikuwa ameshamuelekeza aende Kilimanjaro kuripoti, jana alitakiwa aje kwetu ili tuje tumhoji kwa niaba ya wale kule, lakini tukakuta anaratiba zingine tukaona tupishe ratiba zake watahangaika wenyewe ambako alitendea makosa kwa Dar es Salaam hajafanya makosa", amesema Kamanda Mambosasa. 

Jana Oktoba Mosi, 2020, Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, SACP Wambura, alimuandikia barua mgombea urais kupitia CHADEMA Tundu Lissu, kwa lengo la kumfanyia mahojiano kufuatia kauli na matamshi yake ambayo amekuwa akiyatoa akiwa katika shughuli zake za kampeni.