Alhamisi , 10th Sep , 2020

Mgombea mwenza wa Urais kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan, ameuagiza uongozi wa Mkoa wa Mtwara kwa kushirikiana na TAKUKURU, wahakikishe wanazitafuta Bil 20 zilizoliwa na viongozi wa AMCOS ili wakulima wa Korosho wanaodai pesa zao waweze kulipwa.

Mgombea mwenza wa Urais wa CCM, Samia Suluhu Hassan

Mama Samia ametoa kauli hiyo hii leo Septemba 10, 2020, wakati akifanya kampeni za kumnadi mgombea Urais wa chama hicho, Wabunge pamoja na Madiwani wa CCM, ambapo amesema kuwa viongozi wa vyama vya Ushirika wamewadhurumu pesa zao wale wananchi ambao hawajui kusoma na kuandika.

"Tunaelewa kwamba kulikuwa na deni kubwa la Korosho na Serikali tumelipa lote, lakini viongozi wa AMCOS wameangalia nani hawajui kusoma na kuandika pesa zao wakazichukua, naiagiza Serikali ya Mkoa wa Wilaya kila mkulima aliyedhurumiwa na AMCOS kupitia TAKUKURU pesa yao inapatikana", amesema Mama Samia

Aidha Mama Samia amesema kuwa, "Serikali tumelipa deni lote lakini viongozi wa Vyama vya Ushirika wanafanya mambo yasiyoingilika akilini, Dkt Magufuli alishatoa Bilioni 20 kwa malipo ya korosho, zipo Mtwara zitafutwe wapi zimeingia wanaodai walipwe pesa zao".