Ijumaa , 30th Sep , 2016

Serikali imesema kuwa katika mkutano 71 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa umeonesha Tanzania inatekeleza mpango mpya wa maendeleo endelevu kwa kuzitafuta rasilimali ndani ya nchi na kuzifanyia kazi.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Balozi Dkt. Augustine Mahiga.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi, Dkt. Augustine Mahiga, ametoa kauli hiyo leo Jijini Dar es Salaam wakati akitoa taarifa ya mkutano wa 71 wa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa UN, ambao ulifanyika kwa malengo ya kujadili masuala ya jumla hasa yale ambayo yanaleta tishio la usalama wa amani kwa nchi wanachama.

Amesema kati ya mambo waliyojadiliana ni pamoja na tatizo la madawa ya kulevya na tishio la kimataifa la kiugaidi duniani ambalo limepelekea nchi wanachama kuweka mikakati mahususi ya kuhakikisha vyombo vya ulinzi na usalama vinaimarika wakati wote sambamba na kujihami na matishio mbalimbali ya kigaidi.

Wakati huo huo Balozi Mahiga amezungumzia ziara ya siku 3 ya Makamu wa Ris wa Cuba nchini Tanzania Salvador Antonio Valdes Mesa ambaye anatarajiwa kufika nchini siku ya Jumapili ya tarehe 2 Oktoba na ziara hiyo ni kwa ajili ya kuhimarisha mahusiano ya kimaendeleo baina ya nchi hizi mbili, ambazo zina historia ya muda mrefu ya mahusiano mazuri.