Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akitembelea kiwanda cha Kiluwa Still Group cha Mlandizi Pwani Novemba 19, 2016.
“Nilipokuwa hapa mara ya kwanza niliagiza itengenezwe njia ya reli kutoka njia panda ya reli ya kati, lakini pia niliagiza uwekwe umeme wa msongo mkubwa ili kiwanda kiweze kuanza uzalishaji mapema mwakani. Nimefarijika kukuta maagizo haya yametekelezwa kwa kiasi kikubwa isipokuwa hili la umeme,” amesema.
“Mkandarasi ameomba siku 14, nimempa hadi tarehe 7 Desemba ahakikishe umeme unafanya kazi kwa kiwango kinachotakiwa. Sasa hivi wameanza test lakini muda ili transforma iweze kuhimili mzigo mkubwa… hili ni suala la kitaalamu kwa hiyo tuwape muda.”
Mapema, akiwasilisha taarifa fupi, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Eng. Evarist Ndikilo alisema haelewi ni kwa nini mkandarasi huyo anazidi kuomba siku 14 ili kukamilisha wakati aliahidi kuwa 14 za awali zingetosha kukamilisha kazi hiyo.
Kuhusu fidia kwa wananchi na Halmashauri ya Wilaya hiyo, Mkuu huyo wa Mkoa alisema wananchi waliopisha njia wanadai fidia ya sh. milioni 95.76 na Halmashauri inadai sh. milioni 307.26 na kwamba jumla yote inafikia sh. milioni 403.
Alipopewa nafasi na Mkuu wa Mkoa huo ajieleze mbele ya Waziri Mkuu, ambaye amepewa kazi ya kuweka umeme na transforma Mlandizi alisema anahitaji apewe siku 14 ili aweze kukamilisha kazi hiyo
Mkuu wa mkoa wa Pwani mhandisi Evarist Ndikilo akizungumza jambo mbele ya waziri mkuu Kassim Majaliwa alipowasili kiwanda cha Kiluwa
Naye Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya Dekan Group Ltd, Eng. Desderius Luhaga amesema “Kazi kubwa ya umeme tumeshaifanya na hii ni ya umeme wa msongo wa kilovoti 132, na tumeanza kutest umeme katika baadhi ya mitambo hapa kiwandani, lakini tunahitaji siku karibu tano ili transforma ipoe tangu tulipoifunga ndipo iweze kupokea mzigo mkubwa. Kisha tutaanza kuunganisha katika maeneo mengine madogo madogo humu ndani,”
Katika hatua nyingine, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Reli Tanzania (TRL), Bw. Masanja Kadogosa amesema shirika hilo limetumia sh. milioni 863 kukamilisha ujenzi wa reli ya km.5 kutoka njia panda hadi kwenye kiwanda hicho ambapo kati ya hizo km.1.5 zimo ndani ya kiwanda.
Amesema hadi sasa wameshaweka njia nne za reli, moja ikiwa ni mahsusi kwa ajili ya kubeba makaa ya mawe. “Tulilazimika pia kujenga culvert katika eneo moja kwa sababu pailikuwa na shimo kubwa. Tumetumia fedha kidogo kwa sababu tumetumia mafundi wetu badala ya wakandarasi,” ameongeza.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua kiwanda cha kuunganisha magari ya zimamoto na matrekta cha Equator SUMMA kilichopo Mlandizi mkoani Pwani.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Kiluwa Steel Group, Bw. Mohammed Kiluwa alimweleza Waziri Mkuu kuwa anatarajia kuanza uzalishaji Januari, mwakani na kwamba ataajiri wafanyakazi wapatao 200.
“Tunataraji kuanza uzalishaji Januari, mwakani na uzalishaji utakuwa tani 2,000 kwa siku. Ila tumekubaliana na wawekezaji wenzangu tuweke pia viwanda vingine vitatu kwa sababu kutakuwa na umeme wa kutosha.”
“Tunatarajia kufungua viwanda vine vya kutengeneza gypsum powder, pikipiki, nguzo na vifaa vya kufungia nyaya za umeme mkubwa pamoja na tissue. Tuna eneo lingine Mkuranga lakini kule hakuna umeme, kwa hiyo tumepanga kuweka hivyo viwanda hapa kwa sababu tuna eneo la kutosha.”