Jumatatu , 1st Aug , 2016

Waziri Mkuu Kasim Majaliwa, ameziagiza Halmashauri zote nchini kufanya mapitio ya watumishi wa mikataba ili kuona kama wana sifa za kuajiriwa na wale wasiokuwa na sifa basi waondolewe kwenye ajira hizo.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akiwa na baadhi ya viongozi wa Mkoa wa Morogoro.

Waziri Mkuu amesema hayo Mkoani Morogoro Mara baada ya kupokea taarifa ya Mkoa huo iliyosomwa na Mkuu wa Mkoa huo Dkt. Kebwe Steven Kebwe alipowasilini mkoani Morogoro kwa ziara ya siku mbili.

Waziri Mkuu Majaliwa amesema kuwa ametaka ushirikiano wa watumishi pamoja na uwajibikaji katika utoaji wa huduma kwa wananchi na kuondoa migongano ya kiutendaji kwa wakuu wa wilaya na wakurugenzi.

Waziri Mkuu pia amekumbushia suala la Watumishi hewa kumalizima baada ya mwezi Agosti huku akiwataka wakuu wa mikoa kujiridhisha na watumishi wao na kama kuna wanaotengeneza watumishi hewa basi wachukuliwe hatua haraka.

Katika hatua nyingine Waziri Mkuu ameutaka Mkoa huo kuendelea kwa kufanya uzalishaji na kuendelea kuwa ghala la taifa la chakula kama ambavyo serikali imeliteua.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa huo Dkt. Kebwe Steven Kebwe amemuhakikishia Waziri Mkuu mkoa huo utaendela na Uzalishaji wa Chakula na kuendelea kuwa ghala la taifa la Chakula.

Katika hatua nyingine Waziri Mkuu Kassim Majaliwa,amesema Serikali haitasita kuwaondoa katika nyadhifa zao Wakurugenzi wote watakaoshiriki katika kutoa taarifa za uongo kuhusu miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo yao.

“Serikali inatoa fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo ambapo kuna baadhi ya viongozi wamekuwa wakiandika taarifa za uongo kuwa mradi umekamilika wakati haujajengwa, hivyo wakurugenzi watakaoshiriki kutoa taarifa zisizokuwa sahihi wataondolewa,” alisema.

Waziri Mkuu ameyasema hayo jana wakati akipokea taarifa ya mkoa wa Morogoro mara baada ya kuwasili mkoani hapa kwa ziara ya kikazi ya siku tatu.

Alisema alitumia fursa hiyo kutoa wito kwa wakurugenzi katika halmashauri zote nchini kuhakikisha wanatembelea miradi yote inayojengwa katika maeneo yao ili kufanya ukaguzi na kujiridhisha kama thamani yake inalingana na kiasi cha fedha kilichotolewa.

Sauti ya Waziri Mkuu Kasim Majaliwa.