Ijumaa , 3rd Mar , 2017

Rais Dk. John Pombe Magufuli, ameagiza kushikiliwa kwa hati za kusafiria za mwakilishi wa kampuni ya ukandarasi ya Overseas Infranstructure Alliance Private Limited ya India Bw. Rajendra Kumar pamoja na wasaidizi wake.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na wananchi wa Ng’apa mara baada ya kutembelea mradi wa Maji wa eneo hilo ambao unasuasua kukamilika. Rais Dkt. Magufuli ametoa miezi minne kwa Mkandarasi kampuni ya Overseas Infrastructure Alliance Private Limited ya India kuhakikisha kuwa inakamilisha ujenzi wa mradi huo na sio kuleta visingizio

Ameagza hati hizo zishikiliwe mpaka hapo kampuni hiyo itakapokamilisha ujenzi wa mradi wa maji wa Ng'apa Mjini Lindi ambao ulipaswa kuwa umekamilika tangu tarehe 17 Machi, 2015.

Rais Magufuli ametoa agizo hilo leo alipotembelea mradi huo ambao unatarajiwa kuzalisha zaidi ya lita za ujazo milioni 5 za maji kwa siku kwa ajili ya wakazi wa Mji wa Lindi ambao wanakabiliwa na tatizo kubwa la maji.

Sehemu ya Mradi wa Maji wa Ng’apa mkoani Lindi ambao Rais Dkt. Magufuli ametoa miezi minne kwa mkandarasi anayejenga mradi huo ili uweze kukamilika haraka

Rais Magufuli ameelezea kusikitishwa na usimamizi mbaya wa mradi huo ambao tayari kiasi cha Shilingi Bilioni 21.8 zimetolewa kati ya Shilingi Bilioni 29 zilizopangwa kutumika hadi kukamilika kwake, na ameonya kwamba, endapo mradi huo hautakamilika katika kipindi cha miezi 4 kuanzia sasa atachukua hatua dhidi ya wanaopaswa kuusimamia.

"Ikipita miezi minne nisilaumiwe, hatuwezi kukubali wananchi wa Lindi wanashida ya maji, fedha zimetolewa, mkandarasi anaamua kupeleka fedha India, mradi umecheleweshwa kwa miaka miwili na mkandarasi hayupo kwenye eneo la ujenzi halafu mnaopaswa kumsimamia mnamuangalia tu wakati sheria zipo, kwa nini hamkumfukuza muda wote huu?" amehoji Mhe. Rais Magufuli.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akitoa maelekezo kwa Waziri wa Maji Mhandisi Gerson Lwenge kuhakikisha kuwa Mradi wa Maji wa Ng’apa uliopo mkoani Lindi unakamilika ndani ya miezi mine na si vinginevyo.

Mapema akitoa maelezo kuhusu mradi huo Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhandisi Gerson Lwenge amesema mradi huo unatekelezwa kwa mkopo kutoka Benki ya Maendeleo ya Ujerumani (KFW) na Umoja wa Ulaya (EU) ambapo hadi sasa umefikia asilimia 85 na kwamba mkandarasi amesimamisha kazi kutokana na kuishiwa fedha.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akimpongeza Mama Salma Kikwete mara baada ya kuwasalimia wananchi waliokusanyika karibu na mradi wa Maji wa Ng’apa uliopo Mkoani Lindi. Pia Mama Salma Kikwete amemshukuru Rais Dkt. Magufuli kwa kumteua kuwa Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.