Jumatano , 13th Dec , 2017

Kamishna Jenerali wa Magereza nchini, Juma Malewa amesema katika msamaha uliotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli siku ya uhuru Desemba 9, 2017 haukumuhusu msaani wa filamu Elizabeth Michael maarufu kama Lulu.

Jenerali Malewa amefafanua kuwa mchakato wa kuanza kuangalia wafungwa wakupunguziwa vifungo na kusamehewa haukumuhusisha Elizabeth Michael kutokana na yeye kuingia gerezani wakati tayari mchakato wa kuangalia wafungwa wa kusamehewa na kupunguziwa vifungo ulikuwa umeshaisha 

"Msamaha huu haukumuhusu yeye kwa sababu aliingia magereza wakati tayari zoezi hili lilikuwa limekamilika, kwahiyo labda misamaha ijayo kama itakuwepo lakini katika hii haikumuhusu",amesema Kamishna Malewa.

Kamishna Malewa pia ameeleza  kuwa vipo vigezo vingi vinavyoweza  kumfanya mfungwa asamehewe ama kupunguziwa kifungo kutokana na kosa na muda wa kifungo chake na kwamba misamaha inatofautiana kutokana na kosa kama endapo mfungwa atafata taratibu na kuonekana amerekebishika anaweza kupata msamaha na mengine mengi.

Desemba 9 mwaka huu siku ya uhuru kwa mujibu ya ibara ya 45 ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais John Pombe Magufuli alitoa msamaha kwa  wafungwa 61 waliohukumiwa kunyongwa hadi kufa na wawili Nguza Viking (Babu Seya ) na Johnson Nguza (Papii Kocha ) waliohukumiwa kifungo cha maisha jela na wengine kupunguziwa vifungo vyao.