Alhamisi , 21st Jan , 2016

Rais Magufuli ameanza ziara yake ya kwanza mkoani Arusha na kuwaomba watanzania kutoa ushirikiano wa kutosha kwa viongozi na watendaji wa serikali ya awamu ya tano.

Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli amewasili mkoani Arusha na amewaomba watanzania kutoa ushirikiano wa kutosha kwa viongozi na watendaji wa serikali ya awamu ya tano ili waweze kuendelea kutatua kero zinazowakabili ikiwemo ya kutumbua majipu yaliyoshindikana.

Mh Rais Magufuli amesema hayo alipokuwa anazungumza na maelfu ya wananchi waliojitokeza kumpokea ambao walifunga barabara zaidi ya mara tatu wakitaka azungumze nao amewaomba wananchi kutumia vizuri fursa zilizoanza kujitokeza ikiwemo ya kusomesha watoto wao na ameendelea kuwataka watendaji wakiwemo wakuu wa shule kusimamia vizuri fedha zilizotolewa na serikali.

Aidha Magufuli ambaye akiwa njiani pia amejionea kazi ya uboreshaji wa miundombinu ya barabara amesema serikali itaendelea kuboresha miundombinu ya barabara huku akiwakumbusha wakandarasi kumaliza kazi zao kwa wakati na kwa ubora unatakiwa na kwamba hakutakuwa na huruma kwa atakayekwenda kinyume.

Awali alipowasili katika uwanja wa ndege wa Kilimanjaro Magufuli ambaye pia ameelezea kuridhishwa kwake na mapokezi ya wananchi na viongozi wakiwemo wa vyama vya upinzani walioongozwa na Meya wa jiji la Arusha Mstahiki Kalst Lazaro , na madiwani wa kata mbalimbali na wananchi ambao wameelezea kuridhishwa kwao na utendaji wa serikali ya awamu ya tano.