Jeshi la polisi kitengo cha usalama barabarani mkoani Singida wameanza rasmi kuwapima na kukagua mabasi, kwa madereva wote wanao endesha magari ya abiria yanayoenda nje ya mkoa na ndani ya mkoa wa Singida kama wametumia kileo, ili kuweza kudhibiti ajali ambazo zimekuwa zikitokea hasa wakati huu wa mwisho wa mwaka.
Akiongea kwa niaba ya kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Singida Kamanda wa kikosi cha usalama barabarani Bwana Mohamedi Likwata amesema nia ya kufanya zoezi hilo ambalo ni endelevu ni kupunguza ajali ambazo zinatokea hasa kwa baadhi ya madereva kutumia vileo na kusababisha ajali ambazo zinasababisha vifo na ulemavu.
Kwa upande wao madereva, abiria pamoja na wananchi waliohojiwa wakati wa zoezi hilo likiendelea, wameliomba jeshi la polisi kuhakikisha ni endelevu na pia waweke vituo vya kuwapima madereva hata katikati ya safari na siyo mwanzoni mwa safari kama jinsi wanavyo fanya sasa ili kuweza kupunguza ajali ambazo siyo za msingi.