Jumatano , 6th Jul , 2016

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa nchi kavu na Majini (SUMATRA), Bw. Gilliard Ngewe amesema mamlaka hiyo imesitisha safari za mabasi ya kampuni ya City Boy kutoa huduma ya usafirishaji abiria.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa nchi kavu na Majini (SUMATRA), Bw. Gilliard Ngewe amesema mamlaka hiyo imesitisha safari za mabasi ya kampuni ya City Boy kutoa huduma ya usafirishaji abiria kutoka Dar es Salaam kwenda mikoa ya Shinyanga, Mwanza, Kagera,Tanga na Kilimanyaro mpaka mabasi hayo yatakapofanyiwa ukaguzi na mamlaka hiyo kujiridhisha na matengenezo yake.

Mabasi hayo yataruhusiwa kuendelea kutoa huduma ya usafiri katika njia hizo mara baada ya Mamlaka hiyo kupokea taarifa za ukaguzi kutoka kwa wataalamu wake na kikosi cha usalama barabarani zinazothibitisha kuwa mabasi hayo yanakidhi viwango vya ubora na kuwa madereva wake wanazo sifa za kuendesha mabasi hayo.

Wakati huohuo Watu 46 wamepoteza maisha na wengine 73 kujeruhiwa kutokana na ajali tofauti za mabasi ya abiria na magari mengine katika kipindi cha wiki moja iliyopita hapa nchini.

Takwimu hizo zimetolewa na Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Mohamed Mpinga, wakati akiongea na waandishi wa habari ambapo amedai baadhi ya ajali hizo zimesababishwa na uzembe wa madereva na mwendokasi.

Kamanda Mpinga amesema, madereva wamekua wakikiuka kwa makusudi sheria inayowataka kuendesha kwa mwendo usiozidi kilomita 80 kwa saa, baadhi ya abiria kushangilia mwendokasi bila kutoa taarifa kwa vyombo husika na kwa upande mwingine, baadhi ya wamiliki wa magari hayo kuwapa motisha madereva ambao wanavunja sheria, pale wanapowahi kufika vituo vya mwisho na kuwalipia faini pale wanapokosea.