Jumatatu , 29th Jan , 2024

Waziri wa  Maliasili  na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki  ametoa maelekezo mazito  kwa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) na kulitaka  libadilike ili liweze  kuchangia ipasavyo kwenye  uchumi wa taifa  kuipitia utalii na kuhifadhi raslimali  kwa faida ya kizazi cha sasa na baadaye.

Mhe. Kairuki ametoa maelekezo hayo leo Januari 29,2024 kwenye hafla ya uvalishaji cheo na uapisho wa Kamishna  wa uhifadhi,Musa Kuji katika makao makuu ya TANAPA jijini Arusha.

Amesisitiza kuwa  katika kipindi hiki TANAPA linatakiwa kuja na  ubunifu wa hali ya  juu katika kutangaza vivutio vya utalii  na  kubaini mazao mapya  ya utalii ili sekta ya utalii iweze  kufikia lengo la Ilani  ya Chama Cha mapinduzi (CCM) ya  kuwa  na wageni  milioni tano na kuliingizia taifa jumla ya dola  za kimarekani bilioni sita ifikapo  mwaka 2025.

Amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa  maono yake ya kuifungua Tanzania  duniani kupitia Filamu ya The Royal Tour na kuwataka watumishi wa wizara  yake kuchapa kazi ili kuenzi  kwa vitendo  maono ya Rais.

Aidha, amelitaka TANAPA  kukuza na kuimarisha mahusiano na jamii zinazozunguka  hifadhi na mbuga za taifa pia mahusiano na wadau mbalimbali wa  hifadhi na utalii ili kuweza kubadilishana  mawazo na uzoefu katika uhifadhi na kutangaza  vivutio mbalimbali vya utalii duniani pia uendeshaji wa Shirika kwa ujumla wake.

Ameongeza kuwa  katika kufanya kazi watumishi wanatakiwa kuzingatia kushirikiana na kufanya  kazi kama timu mmoja huku wakizingatia taratibu za Serikali  ili kuweza kupata matokea tarajiwa kwa haraka.

Kuhusu  utekelezaji wa miradi ya maendeleo Mhe. Kairuki amesisitiza kutekeleza miradi yote kwa wakati huku akisisitiza  kufuata taratibu zote za manunuzi ya umma  kwa kuzingatia ubora. Pia kuchukua  hatua  mapema wakati wowote inapotokea  changamoto  badala  ya kukaa kimya  na kuruhusu mitandao  kuendelea kupotosha.

Katibu Mkuu wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbas amemtaka Kamishna Kuji  kuwaunganisha watumishi  wote katika  kipindi chake  huku akimsisitiza kumtanguliza Mwenyezi  Mungu. 

Hafla hiyo ilipambwa na kikosi maalum cha wanamuziki kutyoka TANAPA ambacho  kilitumbuiza wimbo maalum wa kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan  kwa kucheza Filamu ya The Royal Tour.