Jumanne , 24th Jan , 2023

Mapigano mapya yamezuka mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, licha ya makubaliano kati ya serikali na makundi ya waasi kumaliza uhasama.

Mapigano kati ya jeshi na waasi wa M23 siku ya Jumanne yanasemekana kusababisha watu wengi kuyakimbia makaazi yao, kwa mujibu wa ripoti za eneo hilo.

 Jeshi halijatoa tamko lolote kuhusiana na mapigano ya hivi karibuni, lakini msemaji wa waasi hao amevishutumu vikosi vya serikali kwa kushambulia maeneo yao wakati wakijiandaa kuondoka zaidi kama ilivyoainishwa katika makubaliano yaliyofikiwa katika mji mkuu wa Angola, Luanda.

Wiki iliyopita huko Davos Rais Félix Tshisekedi alisema kundi hilo la waasi halijiondoi bali "linazunguka na kupelekwa katika maeneo mengine".

Waasi hao wamemshutumu Rais Tshisekedi kwa kuwa na nia ya dhati ya "kuliangamiza kundi la M23" badala ya kutatua mzozo huo kwa njia ya amani.

Umoja wa Mataifa unasema zaidi ya watu 400,000 wameyakimbia makaazi yao katika mzozo huo tangu mwaka jana.