Jumatano , 15th Jul , 2015

Wananchi wa kijiji cha Ikombe Kata ya Matema tarafa ya Ntebela wilayani Kyela Mbeya wameahidi kutoshiriki katika uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu kwa madai kuwa serikali kupitia halmashauri ya wilaya hiyo kutowapeleke huduma rafiki ikiwemo barabara

Mkuu wa wilaya ya Kyela Thea Ntara.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na kituo hiki mara baada ya kufika eneo hilo wasema ni miaka kadhaa serikali imekuwa ikiwapuuza katika kuwapelekea miundombinu rafiki ikiwemo barabara inayounganisha vitongoji vilivyopo kijijini Ikombe kwenda Matema lilipo soko la gulio.

Wamesema licha ya utawala wa mkuu wa mkoa wa Mbeya na mbunge wa Kyela aliyestaafu John Livingstone Mwakipesile kuiasisi na kuilima barabara hiyo kwa hatua za awali lakini katika utawala wa mbunge Dr. Harrison Mwakyembe wameshindwa kuikamilisha barabara hiyo.

Kayombo Madebe mkazi wa Ikombe amesema wamekuwa wakihatarisha maisha yao kwa kupeleka bidhaa sokoni na kwenda kupata huduma muhimu za matibabu zilizopo makao makuu ya kata ya Matema kupitia mitumbwi hali ya kuwa uwezekano wa kulima barabara hiyo upo.

Amesema halmashauri ya Kyela kupitia mawakala wake wamekuwa wakiwachaji ushuru wa soko kila siku ya gulio bila kujali mateso wayapatayo wakati wa kusafirisha bidhaa zao kwa njia ya mitumbwi hasa wakati wa ziwa kuchafuka.

Wamesema kwa hali hiyo hawako tayari kushiriki katika uchaguzi ujao hadi serikali itakapolima na kuikamirisha barabara hiyo na kuwa walisema wao wameonekana si wakazi halisi wa nchi ya Tanzania kutokana na viongozi hao wa Serikali kutowajali kwa miaka mingi.

Mwenyekiti wa kijiji hicho, Methord Kilongo amesema alipeleka ombi hilo kwa maandishi kwenye halmashauri hiyo kuhusu kero na adha waipatayo wananchi na uhitaji wa barabara hiyo ili kunusuru vifo vitokanavyo na usafiri wa majini lakini wamekuwa wakipigwa danadana kila kukicha.

‘’Wananchi wengi wamepoteza maisha yao kwa nyakati tofauti wakisafiri kutoka tarafa ya Mwambao,Ikombe kwenda Matema kwa njia ya maji,tunaiomba Serikali kupitia halmashauri hiyo ione umuhimu wa kuitengeneza barabara hiyo ili kunusuru maisha ya wakazi hao na kukuza pato la kata’’alisema’’

Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Kyela Clement Kasongo hakupatikana ofisini kwake na alipopigiwa simu hakupokea lakini katika taarifa yake ya awali mbali na kukiri kuwepo na kero hiyo, alisema barabara hiyo wameikabidhi kwa wakala wa barabara nchini Tanroads.