Alhamisi , 28th Apr , 2016

Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvivu, Mhe. Mwigulu Nchemba, amesema kuna baadhi ya watumishi wasio waaminifu wanajinufaisha kwa kujipatia kipato kutoka kwa baadhi ya wafugaji wanaoingiza mifugo katika hifadhi za taifa.

Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvivu Mhe. Mwigulu Nchemba

Akizungumza bungeni mjini Dodoma, Mhe. Nchemba amesema kuwa kuna baadhi ya watumishi wanataifisha mifugo inayoingia katika hifadhi za taifa na kuzichukua pesa hizo kwa manufaa yao huku wingine wakitoa pesa na kuachiwa bila hatua yoyote kuchukuliwa.

Mhe. Nchemba amezitaka taasisi za kiserikali husika zinazosimamia masuala ya rushwa na ukiukwaji wa sheria, kushirikiana na wizara hiyo ili kuwachukulia hatua watumishi wote wanaohusika na tuhuma hizo ambazo zinaitia doa serikali.

Aidha, ameongeza kuwa kuna baadhi ya watumishi wanataifisha mifugo hiyo na kisha wao wenyewe kwenda kuinunua kwa bei ya chini na kuwafanya wafugaji kulalamika kuonewa na kusema kuwa mtumishi anaefanya hivyo ajue huo ni ukiukwaji wa sheria za nchi.

Mhe. Nchemba amesema ili kuendesha nchi kwa utawala bora, wizara yake na Wizara ya Maliasili wataendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ya sheria na mipaka yao ili wajue kuwa kuingiza mifugo katika hifadhi ni kinyume cha sheria.

Sauti ya Waziri wa Kilimo,Mifugo na Uvivu Mhe. Mwigulu Nchemba akiongelea watumishi wa serikali wasio waaminifu