Jumanne , 8th Apr , 2025

Korea Kusini itafanya uchaguzi wa rais tarehe 3 Juni, baada ya mahakama ya kikatiba ya nchi hiyo kuunga mkono hoja ya kumwondoa aliyekuwa Rais Yoon Suk Yeol.

Bunge la nchi hiyo lilipitisha hoja ya kumuondoa madarakani Rais Yoon mnamo mwezi Desemba kwa kutangaza sheria ya kijeshi iliyoshtua nchi.

Mahakama iliidhinisha kushtakiwa kwake tarehe 4 Aprili, na hivyo kufungua njia ya kufanyika kwa uchaguzi wa haraka ndani ya siku 60.

Kaimu rais wa nchi hiyo Han Duck-soo alitangaza tarehe ya uchaguzi leo Jumanne, akisema nchi inahitaji kupona haraka na kusonga mbele.

Tangazo la Yoon la sheria ya kijeshi liliitumbukiza Korea Kusini katika hali ya sintofahamu ya kisiasa na kusababisha mgawanyiko mkubwa nchini humo.

Kaimu rais ameomba radhi kwa kuleta mkanganyiko na wasiwasi kwa wananchi katika kipindi cha miezi minne iliyopita

Yoon alirejelea vitisho kutoka kwa vikosi vinavyopinga serikali na Korea Kaskazini alipotangaza sheria ya kijeshi. Lakini baada ya muda mfupi kupita, ilibainika wazi kuwa hatua hiyo haikuchochewa na vitisho vya nje bali matatizo yake ya kisiasa ya ndani.

Ameshtakiwa kwa kosa tofauti la uasi mbele ya mahakama ya jinai.