Jumatano , 17th Dec , 2014

Katibu Mkuu wa CCM Abdulrahman Kinana amewataka viongozi walioshindwa kutatua migogoro ya ardhi wajiuzulu kwa kuwa wameshindwa kutatua kero ambazo wana uwezo wa kuzimaliza.

Katibu mkuu wa CCM Abdulrahman Kinana

Kinana amesema umefika wakati wa viongozi wa juu katika serikali walioshindwa kumaliza migogoro ya ardhi inayoendelea kushamiri kila kukicha kati ya wakulima na wafugaji katika hifadhi na mapori ya akiba huku wao wakiwa wana kula maisha maofisini kujiuzulu nyadhifa zao kwani hakuna sababu ya kuendelea kubaki madarakani wakati wameshindwa kutatua kero ambazo wana uwezo wa kuzimaliza.

Katibu Abdulrahman Kinana ametoa kauli hiyo katika kikao chake na viongozi wa mila wa kabila la maasai na wabunge kutoka mikoa ya Arusha na Manyara kujadili mabadiliko ya tabia nchi na ongezeko la migogoro ya ardhi katika maeneo hayo ikiwemo Loliondo, Kiteto, Simanjiro, Monduli na Longido amesema ni jambo la kushangaza kuona migogoro inaongezeka watu wanapoteza uhai lakini viongozi wanashindwa kutatua migogoro ambayo ipo ndani ya uwezo wao, hivyo hawana budi kujiuzulu kwa kushindwa kutekeleza wajibu wao na haoni sababu kwanini wanakuwa wagumu kujiuzulu.

Awali wakiwakilisha malalamiko yao wakazi wa maeneo yenye migogoro wamesema wanashindwa kuilewa serikali kwa kuwakumbatia wawekezaji na kuwaacha wananchi wake wakiteseka na kupoteza uhai huku wakazi wa Longido wakitaka serikali iwatafutie mahali pa kuwapeleka kama wanahisi wao siyo watanzania na watu wa Kiteto wakilalamikia baadhi ya viongozi wa CCM kutumia eneo lao kwa mtaji wa kisiasa.

Mbunge wa Simanjiro Christopher Ole Sendeka amemwomba Kinana aingilie kati migogoro ya kijiji cha Kimotoroko na pori la akiba la mkungunero na kudai kuwa mgogoro wa Kiteto unawahusisha watu wakubwa serikalini wakiwemo mawaziri hivyo hauwezi kumalizwa na viongozi wa wilaya hata mkoa huku akimwomba auangalie kwa kina mgogoro huo.