Jumanne , 12th Apr , 2016

Kijiji cha Olbili ,kata ya Sambari wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara kinakabiliwa na tatizo la ukosefu chakula cha miongoni mwa familia nyingi hali inayochangia kuzorota kwa hali ya lishe na shughuli za kijamii pamoja na za kiuchumi.

Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Dkt. Joel Bendera

Wakizungumza naEast Africa radio, wananchi wa kijiji hicho wamesema kuwa uhaba huo wa chakula unatokana na kunyang`anywa maeneo waliyokua wanatumia kwa kilimo na kutumika kama ardhi ya malisho.

Wananchi hao waliandamana na mabango yao kuzunguka eneo la shamba hilo wameiomba serikali kupitia wizara ya ardhi na wizara ya kilimo kuingilia kati mgogoro huo baina yao na wafugaji wanaogombea eneo hilo ambalo kwa zaidi ya miaka 24 tangu mwaka 1992 hadi mwaka 2013 ambapo walizuiwa kutumia maeneo hayo ambayo walikua wakiyatumia kwa shughuli za kilimo cha kujikimu.

Eliud Jackson ni Mwanakijiji wa Olbili amesema kuwa licha ya kunyimwa maeneo ya kulima pia mwaka huu hawakupata chakula cha msaada kama kata nyingine zilizopata mgao huo hivyo kuteseka na njaa wao na watoto wao ,wamemuomba Rais Magufuli kutazama suala hilo na kulipatia ufumbuzi.

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Tilili Kingi Lomayani Laizer amesema kuwa baada ya kuzuiliwa kulima na Mtendaji wa Kata na Diwani aliyekua madarakani walifika katika ngazi za wilaya bila mafanikio hivyo wanamuomba Mkuu wa Mkoa wa Manyara afike kutatua mgogoro huo ili kuwanusuru na baa la njaa.