Alhamisi , 9th Oct , 2014

Hatimaye Rais Jakaya Kikwete na Rais wa Zanzibar wamekabidhiwa katiba iliyopendekezwa na Bunge Maalum la Katiba katika uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma, Dodoma

Mwenyekiti wa #BungeLaKatiba Mh Sitta akimkabidhi Rais @jmkikwete katiba inayopendekezwa

Rais wa Jamuhuri ya muungano wa Tanzania Dk Jakaya Mrisho Kikwete na Rais wa serikali ya mapinduzi ya Zanzibar Dk Ali Mohamed Shein wamekabidhiwa katiba iliyopendekezwa na Bunge Maalum la Katiba ikiwa ni hatua muhimu katika historia ya Tanzania kuelekea kupata katiba mpya ambayo kwa mara ya kwanza imehusisha maoni ya wananchi, makundi maalum, taasisi wanasiasa na viongozi mbalimbali tangu taifa kupata uhuru wake.

Majira ya saa Sita na nusu mchana ndipo makundi mbalimbali ya wageni waalikwa, viongozi wa juu wa serikali mabalozi marais na mawaziri wa kuu wastaafu wakaingia katika viwanja vya Jamuhuri na kisha majira ya saa Tisa na nusu Rais wa serikali ya mapinduzi ya Zanzibar Dk Ali Mohamed Shein akawasili na kufuatiwa na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mara baada ya itifaki ya uongozi kuwasili shughuli ikaanza rasmi ambapo mwenyekiti wa kamati ya uandishi ya Bunge Maalum Mhe Adrew Chenge akaelezea maudhui ya katiba iliyopendekezwa pamoja na mambo mengine akasema katiba hiyo ina jumla ya sura 19 na ibara 296 na nyongeza tatu ambapo rasimu ya awali iliyowasilishwa bungeni ilikuwa na sura 17 na ibara 211 huku suala la muundo wa serikali likisalia kuwa serikali mbili.

Mh Andrew Chenge, ametoa maelezo kuhusu kilichomo ndani ya Katiba inayopendekezwa na kusema kuwa Katiba inayopendekezwa kwa 81.8% inatokana na Rasimu ya Katiba ya Jaji Warioba, na 18.2% pekee ndiyo mambo mapya yaliyoibuliwa wajumbe wa Bunge Maalum.

Nao wawakilishi wa makundi 15 ya kijamii yaliyoshiriki katika bunge hilo maalum la katiba walipata fursa ya kuelezea namna walivyowakilisha na kile walichokubaliana kiwepo katika katiba mpya.

Na kisha kile ambacho kilikuwa kikisubiriwa katika hastoria ya taifa kikawadia ambapo aliyekuwa mwenyekiti wa bunge maalum akakabidhi Katiba iliyopendekezwa kwa Rais Dk Jakaya Kikwete na Rais wa Zanzibar Dk Ali Muhamad Shein.

Baada ya makabidhiano hayo viongozi hao wakuu wa taifa wakaeleza kuhusu mchakato wa katiba ambapo wameelezea matumaini yao makubwa kuhusu katiba hiyo pendekezwa.

Baadhi ya makundi yaliyohudhuria ni pamoja na makundi ya dini, wakulima, wafugaji, wavuvi, elimu ya juu, wanawake, vijana, wasanii, viongozi mbalimbali wa vyama vya siasa na serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na serikali ya mapinduzi Zanzibar pamoja na mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini.

Baadhi ya mabalozi waliohudhuria ni pamoja na balozi wa DRC, Algeria, Angola, Burundi China, India, Indoneseia, Malawi, Nigeria, Palestina, Rwanda, Afrika Kusini, Umoja wa falme za Kiarabu, Zambia, Zimbabwe na Iran.

Miongoni mwa mambo yaliyofanyika leo ni pamoja na Salam kutoka kwa makundi mbalimbali, Utenzi maalum, nyimbo kutoka kwa wasanii na wabunge wanawake, utenzi kutoka na Mrisho Mpoto, Hotuba za marais Dkt Kikwete na Dkt Shein pamoja na tukio kuu ambalo ni la mwenyekiti wa Bunge Maalum Mh Samwel Sitta kukabidh Katiba inayopendekezwa kwa marais hao.

Nao baadhi ya wananchi waliohudhuria siku hii hadhimu kwa mustakabali wa taifa walitoa maoni yao kuhusu mchakato mzima wa uundwaji wa katiba mpya huku wakiwataka watanzania kuwa watulivu katika kipindi chote na watumie vizuri kura ya maoni ili kupata katiba itakayokuwa suluhu ya kutatua changamoto zinazolikabili taifa na yenye mrego wa kimaendeleo.