Jumanne , 25th Nov , 2014

Jaji Joseph Warioba ameendelea kuikosoa Katiba Inayopendekezwa na kusema licha ya kuwa na mambo kadhaa mazuri kama vile Malengo Makuu na Haki za Binadamu, sehemu kubwa ya Katiba hiyo haifai.

Baadhi ya wajumbe wa iliyokuwa tume ya mabadiliko ya katiba wameitaka serikali ichapishe kwa wingi na kuzisambaza kwa wananchi nakala za katiba pendekezwa, ili wananchi waisome, waitafakari na kuielewa kabla ya kuipigia kura ya maoni huku wakitahadharisha uwezekano wa nchi kuwa na katiba isiyokidhi matarajio na maslahi ya wananchi endapo wataipigia kura kabla ya kuisoma na kuielewa.

Wakizungumza katika mdahalo ulioandaliwa na Taasisi ya Mwalimu Nyerere uliofanyika jijini Dar es Salaam wajumbe hao akiwemo aliyekuwa mwenyekiti wa tume hiyo Jaji mstaafu Joseph Warioba, wameelezea kutoridhishwa na Tunu za Taifa, haki za makundi mbalimbali kama vile watu wenye ulemavu, wanawake na watoto baadhi ya vipengele kuondolewa.

Jaji Joseph Warioba ameendelea kuikosoa Katiba Inayopendekezwa na kusema licha ya kuwa na mambo kadhaa mazuri kama vile Malengo Makuu na Haki za Binadamu, sehemu kubwa ya Katiba hiyo haifai na kwamba hata hayo maeneo mazuri yameondolewa vifungu muhimu na kumbana mwananchi asidai mahakamani.

Amesema katiba hiyo haitoi uhakika wa usawa wa kijinsia wa 50 kwa 50 katika nafasi za uongozi hususani nafasi za ubunge.

Akizungumza katika mdahalo huo aliyekuwa mjumbe wa tume Bw Hamfrey Polepole ametaka kuwepo maridhiano ya kikatiba kati ya pande mbili za muungano ili uwepo muungano unaokubaliwa, unaodumishwa na kulindwa kikatiba huku akieleza kusikitishwa na kitendo cha kufutwa kwa ibara muhimu zilizokuwa katika rasimu ya katiba na kushauri ibara hizo zirejeshwe kwani ndiyo msingi wa katiba inayozingatia maslahi ya wananchi na taifa imara.

Baadhi ya wananchi na viongozi wa kisiasa waliohudhuria mdahalo huo na kupata fursa ya kuuliza maswali akiwemo Prof Ibrahimu Lipumba amesema katiba isiyozingatia maadili na kuweka bayana tunu za taifa haiwezi kuwa katiba bora itakayodumu kwa miaka mingi ijayo huku baadhi ya wananchi wakiomba ufafanuzi kwa baadhi ya vipengele vilivyopo kwenye rasimu ya pili hasa kile kinachohusu madaraka ya rais.

Hata hivyo mdahalo huo umekuwa na ulinzi mkali wa polisi tofauti na midahalo mingine ambapo EATV imeshuhudia wahudhuriaji wakiwa wanakaguliwa na vifaa maalum kabla ya kuingia ndani.