Jumatano , 5th Nov , 2014

Jeshi la Polisi nchini Tanzania Kikosi cha Usalama Barabarani, kimewasilisha kanuni Nne mpya za ukaguzi wa magari nchini ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kukabiliana na Ongezeko la ajali za barabani hususani kwa magari yanayosafirisha abiria nchini.

Kamanda wa Polisi wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini Tanzania,Kamanda Mohamed Mpinga

Wakati akifungua majadiliano ya namna kanuni hizo zitakavyosaidia kukabiliana na ajali hizo, Kamanda wa Polisi wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini Tanzania, Kamanda Mohamed Mpinga amesema kanuni hizo zitasaidia kuyabaini magari ambayo yamechakaa kwa kutumia mfumo wa kisasa.

Kwa upande wake aliyekuwa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usafiri wa nchi kavu na Majini SUMATRA, Ahmad Kilima amesema kanuni hizo zitapunguza ajali zisizo za lazima zinazosababishwa na uchakavu wa magari.

Kilima ameongeza kuwa takwimu zinaonesha ajali nyingi zinatokana na magari chakavu ambayo aidha ni matairi mabovu, yametumika muda mrefu na kusema kuwa mpango huo utaweza kupunguza vifo na ulemavu unaotokana na ajali za kizembe kwa kiasi kikubwa.