Jumatano , 27th Jan , 2016

Kamati ya Usuluhishi wa migogoro ya ndani ya Bunge la Afrika Mashariki imewakutanisha wawakilishi serikali ya Burundi, Vyama vya upinzani na Asasi za kiraia kwa lengo la kujadili namna ya kurejesha hali ya utulivu katika nchi hiyo.

Mwenyekiti wa Kamati ya Usuluhishi wa migogoro ya ndani ya Bunge la Afrika Mashariki Abdullah Mwinyi.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo Abdullah Mwinyi amesema kuwa tayari pande zote mbili wamewasili katika majadiliano hayo wakiwemo chama tawala na vyama pinzani vya CNDD na FDD majadiliano ambayo watafanya pamoja na kamati hiyo ambapo matokeo ya majadiliano yatatangazwa rasmi.

Mwinyi alisema kuwa mgogoro huo umechukua muda mrefu na kusababisha mauaji ambayo yanazidi kukithiri kila kukicha hivyo Kamati hiyo imaeamua kuchukua jukumu la usuluhishi wa mgogoro huo ili kuhakikisha kuwa Burundi inakua salama.

Awali Spika wa Bunge la Afrika Mashariki Daniel Kidega amesema kuwa Bunge hilo limechukua hatua ya usuluhishi wa mgogoro wa Burundi kama inavyoelekeza katika mkataba wa jumuiya hiyo unaozitaka nchi mwanachama kuhakikisha kuwa utawala wa demokrasia ,amani na kuheshimu haki za binadamu vitu ambavyo vimekiukwa na nchi hiyo.

Spika amesema kuwa Burundi ikiwa katika hali mbaya hata nchi jirani za Afrika Mashariki zinakua kwenye hali ya mashaka hivyo tumeajikita katika kurejesha hali ya amani nchini humo.

Kamati ya Usuluhishi wa migogoro ya ndani ya Bunge la Afrika Mashariki inaendelea na vikao vya majadiliano juu ya namna ya kurejesha amani katika makao makuu ya jumuiya hiyo jijini Arusha .