
Kamishna Simon Sirro
Hayo yamewekwa hadharani na Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaa Kamishna Simon Sirro alipokuwa kwenye kipindi cha East Africa Breakfast cha EA Radio, na kuwataka wananchi kuwa na utamaduni wa kutoa ushahidi wa kesi wanazofungua ili watu wahalifu hao wafungwe kwa mujibu wa sheria badala ya kulaumu jeshi la polisi.
Amesema kitendo cha wananchi kukwepa kujitokeza kutoa ushahidi wa kuwatia watu hatiani kunaiongezea gharama kubwa jeshi hilo kwa ajili ya kuwatunza, kuwahifadhi na kuwahudumia kwa chakula.
“Unapoendelea kumuweka mahabusu naye ni binadamu anatakiwa kula, kuoga kusafishiwa maliwato na chumba cha kulala gharama zote ni za serikali ndiyo sababu kubwa tunatoa dhamana ili kuepuka gharama”. Amefafanua Kamishna Sirro.
Amesema Watanzania wengi wamekuwa na tabia ya kulaumu jeshi la polisi pale wanapomuona mtuhumiwa aliyekamatwa na vidhibiti akiwa ameachiwa huru pasipo kujua kuwa kesi yoyote lazima itolewe ushahidi ndipo mtuhumiwa aweze kufungwa kwa mujibu wa sheria.
“Watanzania wote utamaduni wa kufika mahakamani hawana, wao wanachojua ni mtu anakamatwa tu na kufikishwa kituoni, wakati inatakiwa uhakikishe mtuhumiwa kafunguliwa mashtaka na mahakamani kapelekwa pia ushahidi katolewa, ukifuatilia hayo hutolalamika eti askari wamepatiwa rushwa". Amesema Sirro